Kigoma. Ni simulizi ya mauaji yenye kuacha mshangao baada ya wanawake wawili kuhukumiwa adhabu ya kifo, mmoja kati yao ni ndugu wa damu aliyekodi muuaji kwa gharama ya Sh70,000 ili kumwekea sumu dada yake.
Mshitakiwa wa pili, Evodia Bazila alimkodi mshitakiwa wa kwanza, Aneth Tabu ambaye ni rafiki wa karibu na marehemu na kumpa ugoro uliochanganywa na sumu akampa ‘besti’ yake na kumuua.
Makubaliano yalikuwa Aneth alilipwa malipo ya awali ya Sh20,000 kati ya Sh70,000 walizokubaliana. Siku ya tukio Mei 5, 2022 mkoani Kigoma, Aneth akampa besti yake sumu.
Hukumu ya adhabu ya kifo imetolewa Septemba 19, 2024 na Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma aliyesema adhabu kwa kosa la mtu anayetiwa hatiani kwa kuua kwa kusudia ni moja, nayo ni kunyongwa hadi kufa.
Katika hukumu, Jaji alianza kwa kusema kama mtu anataka kupata uthibitisho kuwa kuna wakati urafiki unaweza kuishia pabaya basi anapaswa kusoma hukumu ya kesi hiyo namna rafiki alivyotumika kumuua besti yake.
“Mshitakiwa wa kwanza (Aneth) ambaye anakiri kwa kinywa chake kuwa marehemu alikuwa swahiba wake anashitakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya rafiki yake Amina Bazila bila uhalali wowote wa kisheria,” amesema Jaji.
“(Aneth) anashitakiwa pamoja na mdogo wa marehemu Evodia Bazila. Mshitakiwa wa kwanza anakubali mahakamani kumpa rafiki yake ugoro ambao ulichanganywa na sumu ambao alipewa na mshitakiwa wa pili (Evodia),” ameeleza.
Kwa mujibu wa ushahidi ulio katika hukumu ya Jaji Nkwabi, Mei 5, 2022 katika Kijiji cha Bitare wakati Amina Bazila (marehemu) na mshitakiwa wa kwanza, Aneth walikuwa marafiki wakubwa, wakinywa pombe kwenye baa ya Evodia Bazila.
Aneth alikiri kuwa Evodia, alimpa ugoro uliokuwa umechanganywa na sumu ili ampe dada yake ambaye sasa ni marehemu baada ya kukubaliana kuifanya kazi hiyo kwa Sh70,000 na kupewa malipo ya awali ya Sh20,000.
Alifanya kazi hiyo na malipo yaliyobaki angelipwa baadaye, na kiini cha mgogoro kati ya marehemu na ndugu yake kilianzia kwenye mgawanyo wa mali za dada yao Consolata Bazila aliyefariki dunia.
Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza, mshitakiwa wa pili alikuwa amemtishia dada yake kwa kumwambia, “umechukua mali zote basi tutaona.”
“Mshitakiwa wa kwanza (Aneth) alikuwa muwazi sana. Katika maelezo yake ya kukiri kutenda kosa hilo mbele ya mwenyekiti wa kijiji alisema alimpa sumu marehemu baada ya kupewa na mshitakiwa wa pili (Evodia)” alisema Jaji.
“Alikiri katika maelezo yake ya onyo polisi na katika maelezo yake kwa mlinzi wa amani. Hata kwenye utetezi wake, mshitakiwa wa kwanza alikiri kosa kwa maelezo kuwa alifanya kosa hilo kutokana na ulevi na kama siyo pombe asingefanya,” amesema.
Jaji amesema kuhusu kesi dhidi ya mshitakiwa wa kwanza, anachotakiwa kukizingatia ni kama kweli alitenda kosa hilo akiwa amekunywa pombe, hivyo utetezi wa kuwa alikuwa amezidiwa na sumu ya pombe uwe na nguvu.
Kujibu hoja kama mshitakiwa wa kwanza, Aneth alifanya mauaji kwa ushawishi wa pombe, Jaji alichambua kwa kuegemea maswali matano, moja ni kwa nini hakunywa sumu hiyo yeye au Evodia Bazila au hata kumpa mbwa.
Swali la pili alilojiuliza Jaji ni kwa nini alikumbuka namna walivyofanya majadiliano ya kiasi cha kulipwa, malipo ya awali aliyolipwa na kiasi alichokuwa anadai ambacho ndicho kilichomtoa ‘paka kwenye begi’ kwa maana siri kufichuka.
Tatu ni kwa nini alishindwa kumtonya marehemu uwepo wa jambo hilo na badala yake akatekeleza njama waliyokula pamoja na mshitakiwa wa pili; na nne ni kwa nini alimsubiri marehemu kwenye baa anayojua alikuwa mteja.
Katika swali la tano, Jaji alisema mshitakiwa ndiye alimsubiri marehemu hadi alipoomba ugoro ili asiweze kumtilia shaka na kuwepo hapo kuhakikisha anauvuta ugoro uliokuwa na sumu aliopewa na Evodia Bazila.
Jaji amesema ni wazi kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka kwamba, marehemu alikufa kutokana na sumu kwa sababu sampuli za utumbo na ini vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kuthibitisha uwepo wa sumu.
“Ushahidi uko wazi kabisa kuwa mshitakiwa wa kwanza alikuwa na dhamira ya kumuua marehemu kwa sumu. Kwa kweli hiyo ni silaha hatari kama ilivyo bunduki inavyoweza kuua. Kwa kumpa ile simu alikuwa na dhamira ya kuua,” amesema Jaji.
Amesema anachokiona ni kuwa, kunywa pombe ni kufanya mpango wake uonekane una uhalisia na kumfanya marehemu asishuku lolote na pia jamii isimshuku wala Mahakama, kwa hiyo utetezi wa ulevi unakataliwa.
Katika utetezi wake, mshitakiwa wa pili, Evodia Bazila alikana kuhusika na mipango ya kumuua dada yake kwa sumu na kwamba, mshitakiwa wa kwanza atakuwa ameamua kumhusisha kutokana na mgogoro baina yao wawili hao.
Mgogoro huo ulitokana na mshitakiwa wa kwanza kumtuhumu Evodia kuwa na mahusiano na mume wake, na kwamba alikuwa amemsaidia mumewe huyo kuwa na mahusiano na wanawake wengine.
“Alieleza kuwa siku ya tukio, marehemu na mshitakiwa wa kwanza hawakuwahi kwenda kwenye baa yake kunywa pombe za kienyeji. Kiuhalisia anasema siku hiyo alikuwa anaandaa pombe ambayo ingenywewa siku inayofuata,” ameeleza Jaji.
Kama huo ndiyo ushahidi wa pande mbili kumhusu mshitakiwa huyo, Jaji amesema ni wajibu wa Mahakama kujibu hoja mbili, kama mshitakiwa huyo alipanga njama za kumuua marehemu kwa sumu, na kama anawajibika kwa mauaji hayo.
Jaji amesema kwa kuanzia, ushahidi wa shahidi wa pili, Michael Nakumutu alieleza siku ya tukio alimuona marehemu katika baa ya mshitakiwa huyo na ilikuwa muda wa saa 1.45 usiku ndiyo marehemu aliondoka na kurudi nyumbani.
“Ni wazi kuwa mshitakiwa wa pili aliidanganya Mahakama katika utetezi wake na ushahidi wa shahidi wa pili na wa kwanza unaunganika kuthibitisha siku ya tukio marehemu alikwenda kunywa pombe katika baa hiyo,” amesema.
Jaji Nkwabi amesema kipande hicho cha ushahidi kinashabihiana na alichosema mshitakiwa wa kwanza katika maelezo yake ya kutenda kosa hilo aliyoyatoa Polisi na maelezo ya onyo kwa mlinzi wa amani.
Sehemu ya maelezo hayo yanasomeka: “Nilimuua Amina Bazila kwa sumu. Ilikuwa ni Jumanne sikumbuki tarehe tuliyokuwa tunakunywa. Nililewa. Nilikuwa na Evodia katika baa iliyopo eneo la Kijiji cha Bitare.”
“Evodia alinipa kitu kwenye ugoro ili nimpe Amina Bazila kwa sababu alikuwa ni rafiki yangu wa karibu. Nikaenda kumtafuta Amina nikamkuta anakunywa pombe. Amina akaniomba ugoro ili avute nikampa (ule aliopewa na Evodia)”
Jaji amesema ukiacha ushahidi huo, sababu ya mshitakiwa wa pili kutokwenda kumuangalia dada yake alipokuwa mahututi inazua maswali licha ya kudai alikuwa katika msongo wa mawazo na ana tatizo la moyo kupanuka.
“Alipobanwa (na mawakili wa Jamhuri) atoe vithibitisho vya ugonjwa alibadilisha hadithi yake na kusema haikuwa lazima kwake kwenda kumjulia hali dada yake kwa kuwa kulikuwa na watu wengi wa kumwangalia,” amesema Jaji Nkwabi.
Jaji amesema kitendo cha kushindwa kuwasilisha vielelezo vya ugonjwa wake mahakamani wakati anakabiliwa na shitaka zito la mauaji lilikuwa jambo la kutilia shaka maelezo yake kwani kulihitajika ushahidi kuthibitisha anachosema.
“Kubadili hadithi yake kunafanya aonekane ni muongo na kufanya kesi ya Jamhuri iwe na mizizi. Yaani alienda mbali na kubisha hata kumuona mshitakiwa wa kwanza pale Bitare ambako mshitakiwa wa kwanza anasisitiza alienda,” amesema.
Kutokana na uchambuzi wa ushahidi huo na ushahidi dhidi ya mshitakiwa wa kwanza, Jaji Nkwabi amesema washitakiwa wana hatia ya kuua kwa kukusudia na adhabu ya kosa hilo ni moja, nayo ni kunyongwa hadi kufa.