Rais Mwinyi aipongeza Airpay uzinduzi wa mifumo ya kidijitali ya ZEEA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ally Mwinyi (kushoto) akimkabidhi tuzo Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Airpay Tanzania Yasmin Chali (kulia) kwa kudhamini Tamasha la Pili la Fahari ya Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Kampuni ya Airpay Tanzania kwa kudhamini Tamasha la pili la Fahari ya Zanzibar lililoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA)kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata mikopo, mafunzo ya ujasilimali kwa njia ya kidigitali.

Rais Mwinyi ametoa pongezi hizo leo visiwani Zanzibar wakati akifungua tamasha hilo lililoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) chini ya ufadhili wa Airpay na kuwakutanisha zaidi ya wajasiriamali zaidi ya 200 huko Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Katika tamasha Rais Mwinyi amezindua mifumo mitatu ya ZEEA ikiwemo wa utoaji mikopo kwa njia ya kieletroniki, mfumo wa ZEEA Shop pamoja na ZEEA mafunzo yote ikiwa imeandaliwa na kampuni ya Airpay Tanzania.

Akiwa katika tamasha hilo Rais Mwinyi ameipongeza Airpay na wadhamini wengine waliofanikisha tamasha hilo na kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga bajeti ya Sh. Bilioni 41.6 kwa lengo la kuongeza nguvu katika utekelezaji wa dhamira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“ZEEA tangu kuanzishwa kwake katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili imewezesha upatikanaji wa mitaji pamoja na kuimarika kwa marejesho sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali pamoja kuwaunganisha na masoko ya ndani nan je ya nchi,” amesema Rais Mwinyi

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airpay Tanzania, Yasmin Chali amesema Airpay kwa kushirikiana na ZEEA imeanzisha mfumo maalumu utakaowasaidia wajasiriamali kupata mikopo kidigitali kwa muda mfupi na rahisi.

Chali amesema kwa sasa wajasiriamali wataondokana kujaza makaratisi kwa ajili ya kuomba mikopo na badala yake watatumia simu zao ama mtandao kwa ajili ya kuomba mkopo ili kukuza na kuboresha biashara zao

“Mfumo huu utawafikia wajasiriamali wengi zaidi hivyo niwaombe wafanyabishara wote kuutumia ili kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao, tutatoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa walengo ili waweze kutumia bila kikwazo cha aina yeyote ile,” amesena

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji ZEEA, Juma Burhan amesema wakala huo utaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ili kufikia lengo la kupunguza umaskini kwa wananchi wa Zanzibar.

Amesema wakala kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali katika wilaya zote za unguja na Pemba ili kukuza mitaji ya kuendesha biashara zao.

Related Posts