Rais Samia aihakikishia JWTZ hali nzuri wakati wote

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itahakikisha wanajeshi wanapitia nyakati nzuri wakati wote.

Kauli hiyo inatokana na kile alichoeleza kuwa, anatambua kwa sasa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuna muda linapitia nyakati mbaya na nzuri.

Rais Samia ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ametoa kauli hiyo wakati akiwapongeza watumishi wa JWTZ kwa kazi ya ulinzi  wa mipaka na Katiba.

Rais Samia amesema hayo leo Septemba 20, 2024 alipohojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ.

“Niwaambie wanajeshi najua kuna wakati mnapitia nyakati nzuri na mbaya, lakini tutahakikisha kuona mnapitia hali nzuri wakati wote,” amesema.

Katika mahojiano hayo na TBC, Rais Samia amesema miaka 60 ya JWTZ ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wasimamizi wa jeshi hilo, wakiwamo wakuu wa majeshi tangu uhuru hadi sasa.

Amesema mafanikio hayo pia ni vigumu kuyatenganisha na ufanisi wa mawaziri waliopita katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tangu enzi za uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Katika kila kinachofanywa na jeshi hilo, Rais Samia amesema Serikali ipo pamoja nalo na inafanya kila namna kuhakikisha analiwezesha kwa vifaa na mahitaji mengine.

Kwa jumla, amesema ndani ya miaka 60 JWTZ limepitia safari ndefu.

“Lakini napongeza kwamba katika kipindi chote Jeshi limefanya kazi nzuri ya kulinda nchi, mipaka na Katiba,” amesema.

Amesema kuna mambo mengi yamefanywa ndani na nje ya Tanzania kupitia jeshi hilo.

Kwa upande wa ndani, amesema wakati wote jeshi limekuwa mwokozi yanapotokea maafa na majanga mbalimbali.

Amesema JWTZ linafanya kazi za kusaidia shughuli za kiraia, kwa mfano maafa ya mazingira, kuzama kwa meli na hata maradhi.

Kuhusu Katiba na mipaka ya nchi, amesema imeendelea kulindwa na jeshi hilo ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya ndani ya nchi.

“Tanzania inazungukwa na nchi saba hadi nane na jeshi ndilo lenye kazi ya kuhakikisha mipaka yote iko salama.

“Kuna mipaka ya ardhini na kuna ile ya majini na angani, yote hii inalindwa na jeshi letu na imekuwa salama,” amesema.

Kwa upande wa nje ya Tanzania, amesema JWTZ limeshiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi wa amani katika mataifa mbalimbali.

Amesema limeshiriki kupitia vikosi vya amani vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na hata kujitolea kama Taifa.

Rais Samia amesema jeshi hilo pia linawalea vijana kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na linatumika kujijengea nyumba zake za makazi.

“Hivi sasa kuna kandarasi nyingi ambazo zinafanywa na jeshi kwa hiyo limekuwa likisaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema.

Related Posts