WAKALI wao., Tausi Royals inazidi kutishia vigogo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) upande wanawake, baada ya kuifunga DB Lioness kwa pointi 61-51 kwenye mchezo mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay,
Tausi Royals ambayo ni timu ngeni katika ligi hiyo, imebakiza michezo miwili dhidi ya Vijana Queens na Polisi Stars ili ikamilishe michezo 30 ya mzunguko wa pili.
Katika msimamo wa ligi hiyo kwa upande wa wanawake, Tausi Royals inashika nafasi ya pili kwa pointi 51, huku DB Troncatti ikiwa ndio kinara kwa kukusanya pointi 53.
Tausi Royals inayoundwa na wachezaji nyota waliowahi kuchezea Vijana Queens kama Diana Mwendi na Tukusubira Mwalusamba, ilianza mchezo katika robo ya kwanza kwa kasi hali iliyofanya iongoze kwa pointi 13-3.
Robo ya pili DB Lioness ikimtumia Taudencia Katumbi raia wa Kenya ilifunga pointi 21-16 na hadi kufikia mapumziko Tausi Royals ilikuwa mbele kwa pointi 29-24.
Katika mchezo huo, Diana Mwendi aliongoza kwa kufunga pointi 18, kati ya pointi hizo alifunga katika maeneo ya mitupo ya pointi tatu akivuna pointi 12.