Tumetoka mbali. Hivi ndivyo unavyoweza kueleza safari ya mabadiliko ya sekta ya usafiri wa abiria hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
Kutoka kupanda mabasi ya UDA yaliyohodhi usafiri, Dar ilifika mahala ikajaa abiria, mabasi ya UDA na mengineyo yaliyokuwepo hayakuhimili vishindo vya wingi wa abiria.
Kunusuru hali hiyo, mwanzoni mwa miaka ya 1990, Serikali ikaja na mpango wa kuruhusu watu binafsi kutoa huduma hiyo.
Baadhi walioitika wito huo wakatumia mpaka malori madogo hasa aina ya canter na mengineyo ya muundo wa pickup, na kuyawekea viti vilivyokuwa vikiangaliana.
Huu ukawa mwanzo wa kuja kwa magari ya abiria yaliyopachikwa jina la Chai Maharage. Unajua kwa nini Chai Maharage?
Umeshawahi kwenda katika kibanda cha mama ntilie kuagiza chai na chapati? Kama hukuwahi ni hivi vibanda vingi zamani na hata sasa hujengwa katika mtindo ambao wateja wanapata huduma wakiwa wameangaliana, aghalabu wateja hukaa juu ya mabenchi wakitazamana huku wakipata chai, chapati, maharage na kadhalika.
Waswahili hawakuwa na dogo wakachukua sura hii ya vibanda vya kuuza chao na maharage na kuvipeleka kwenye magari. Na kwa hakika hawakukosea, kuna mfanano mkubwa!
Leo tunavyoringia mabasi ya mwendo kasi, mabasi ya kisasa zaidi ndani ya miji na hata yanayosafiri mikoani, tukumbuke tumetoka mbali.