Jumla ya watumishi 49 kutoka halmashauri 12, wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kuratibu Vikao vya Bodi na Menejimenti (e-Board).
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mamalaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) yamefanyika kuanzia Septemba 18 hadi 20 mwaka huu mjini Morogoro, na kuwahusisha Maafisa TEHAMA, Maafisa wanaohusika na kuratibu vikao vya Bodi, Menejimenti na Madiwani, Maafisa kutoka Idara ya Utawala na wajumbe kutoka kwenye Menejimenti.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo Afisa TEHAMA kutoka e-GA Bi. Khadija Mzenzi amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa juu ya matumzi sahihi ya mfumo wa e-Board, ili halmashauri hizo ziweze kuratibu uendeshaji wa vikao vya Bodi, Menejimenti na Madiwani kwa njia ya kidigiti.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza e-GA kwa ujenzi wa mfumo huo ambao unalenga kuongeza ufanisi wa uandaaji na uendeshaji wa vikao sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji.
Afisa Tawala Wilaya ya Busega Bw. Meshack John, amesema kuwa, ni vema halmashauri zote zikaanza kutumia mfumo huo ili kurahisisha shughuli za uandaaji na uendeshaji wa vikao ndani ya halmashauri.
Naye Mkuu wa Idara ya TEHAMA Manispaa ya Temeke Bw. Yahya Madenge amesema kuwa, mfumo wa e-Board ni miongoni mwa jitihada znazofanywa na e-GA za kuhakikisha shughuli zote za utendaji kazi ndani ya taasisi za umma zinafanyika kidijiti ikiwemo uendeshaji wa vikao.
“Kutokana na mafunzo tuliyopata Mfumo wa e-Board unadhamiria kutusaidia sisi watendaji kuendesha vikao kwa urahisi zaidi na kuwenza kutunza kumbukumbu kwa ufasaha, na hii ni miongoni mwa malengo ya e-GA ya kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanaimarika”, amefafanua Bw. Madenge.
Aidha, Afisa ufuatiliaji na tathimini Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi. Christa Manyalla na Katibu wa Mikutano Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Gudika kimboka wamesema kuwa, mfumo huo wa e-Board utakwenda kuwa msaada mkubwa katika kupunguza gharama na kurahisisha uandaaji wa vikao vya Bodi na Menejimenti katika halmshauri hizo.
The post 𝗛𝗔𝗟𝗠𝗔𝗦𝗛𝗔𝗨𝗥𝗜 𝟭𝟮 𝗭𝗔𝗣𝗔𝗧𝗜𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗙𝗨𝗡𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗠𝗙𝗨𝗠𝗢 𝗪𝗔 𝗲-𝗕𝗢𝗔𝗥𝗗 appeared first on Mzalendo.