Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya dereva bodaboda wilayani Nanyumbu aliyejulkana kwa jina la Aziz Alumen Njombi (30).
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amesema kuwa mwili wa Njombi umekutwa katika kijiji cha Naisero wakati yeye ni mkazi wa kijiji cha Mangaka wilayan Nanyumbu mkoani Mtwara.
Amesema marehemu alikuwa dereva bodaboda katika kijiwe cha Jangwani ambapo siku ya Septemba 19,2024 saa tatu usiku akiwa na pikipiki yake yenye namba za usajili MC827EHW, alikodiwa na watu ambapo hawajafamika mpaka sasa.
“Hili sio jambo la kawaida yaani mwili umekutwa Septemba 20, 2024 saa tatu asubuhi ukiwa umetelekezwa porini, eneo ambalo halina makazi ya watu ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na pikipiki ikiwa haipo huu ni ukatili ambao tunapaswa kuukemea” amesema Suleiman.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za kweli na uhakika kuhusu tukio hili asisite kuiwasilisha kwa polisi au mamlaka yoyote atakayeona inafaa, ili asaidie kuwakamata waliohusika na mauaji hayo ya kikatili.
Mwenyekiti wa umoja wa chama cha madereva bodaboda Wilaya ya Nanyumbu Mussa Kachinja (Banzi) amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya usiku wa tukio kutoka kwa mke wa marehemu juu ya kupigiwa simu na mtu akidai namba ya siri ya simu ya mumewe walipata hofu.
Hata hivyo, walijaribu kwenda kituo cha polisi na kutoa maelezo kisha kurejea nyumbani ambapo kesho yake asubuhi walianza msako wa kumtafuta mwenzao.
“Juzi saa saba usiku mke wa marehemu alipigiwa simu na mtu asiyemjua aliyejitambulisha kwa jina la Said kwa kutumia simu ya mumewe aliomba namba ya siri ya simu ya mume wake (smartphone) na kudai kuwa amemfumania na amempiga hajiwezi, hivyo anataka namba hiyo aangalie simu ambapo mke alijibu kuwa haijui simu ikakatwa hali ambayo ilisababisha mke wake kutoa taarifa kwa ndugu na marafiki
“Tulianza oparesheni ya kumtafuta marehemu tuligawanyika makundi ambapo kundi moja lilibaini uwepo wa damu chini ya daraja, tulipoifuatilia hadi mwishoni tuliona ndala na baadaye mwili ukiwa umetelekezwa porini” .” amesema Kachinja
Matukio kama haya yamekuwa yakijitokeza na ndani ya miaka mitatu, zaidi ya waendesha bodaboda watano wameuawa.
Naye Diwani wa kata ya kilima hewa wilayani Nanyumbu (CCM) Thabiti Geugeu amesema kuwa tukio hili limewasikitisha kwa kuwa marehemu alikuwa akitelekeza majukumu yake ya kujitafutia riziki.
“Tumepokea kwa masikitiko kifo hiki matukio haya sio mazuri ni vema sasa bodaboda waache kupakia watu wasiowafahamu hasa usiku na kuwapeleka nje ya mji. Hii kwao sio ishara nzuri kwao ni vema tukakemea kwa sauti kubwa ili vitendo hivi visijirudie,’’ amesema.