CAF yamaliza utata, Simba bado tishio Afrika

CHATI ya Caf ya ubora wa klabu hupangwa kwa kuzingatia pointi ambazo klabu imekusanya katika ushiriki wake kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa kipindi cha misimu mitano ya nyuma.

Kwa mujibu wa Caf, timu huanza kuhesabiwa pointi hizo kuanzia hatua ya makundi hadi ile ya fainali na zinazotolewa katika raundi ya kwanza na ya pili hazipati pointi yoyote.

Kwa mujibu wa muongozo wa sasa, ushiriki wa kuanzia hatua ya makundi hadi fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika unakuwa na idadi kubwa ya pointi kulinganisha na ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, bingwa anapata pointi sita (6), mshindi wa pili anapata pointi tano (5), timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi nne, pointi tatu ni kwa timu inayotolewa katika robo fainali, timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata pointi mbili na pointi moja hupata timu ambayo inashika mkia kwenye kundi.

Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika,timu ambayo inashika mkia kwenye kundi inapata pointi 0.5, timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata pointi moja (1), pointi mbili (2) ni kwa timu inayotolewa katika robo fainali,  timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi tatu (3), mshindi wa pili anapata pointi nne (4) na  bingwa anapata pointi tano (5).

Kisha pointi hizo zinazidishwa kwa alama ya msimu mmoja mmoja katika mitano iliyopita ambao msimu wa tano nyuma unakuwa ni alama moja, msimu wa nne unakuwa ni alama mbili, msimu wa tatu unakuwa ni alama tatu, msimu wa pili nyuma unakuwa ni alama nne na msimu mmoja nyuma unakuwa ni alama tano.

Mfano kwa sasa, msimu mmoja nyuma ni 2023/2024, msimu wa pili nyuma ni 2022/2023, msimu wa tatu nyuma ni 2021/2022, msimu wa nne nyuma ni 2020/2021 na msimu wa tano nyuma ni 2019/2020 mtawalia.

Timu iliyochukua taji la Ligi ya mabingwa msimu uliopita, ilipata pointi sita ambazo kwa vile ni msimu mmoja nyuma, zinazidishwa kwa tano hivyo timu kwa msimu huu inakuwa ina pointi 30 kwa kupiga hesabu za msimu uliopita tu hivyo kupata pointi za misimu mitano nyuma, hesabu inapigwa kwa kuzidisha pointi ambazo timu imekusanya kwa kila msimu kati ya mitano iliyopita na alama za msimu huo kwa hiyo kisha zinajumlishwa kupata idadi ya pointi ambazo timu imevuna katika kipindi cha misimu mitano nyuma.

VITA YANGA, SIMBA IKO HAPA

Kwa msimu wa sasa, Simba inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 39 na Yanga iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31.

Pointi 39 za Simba imevuna kutoka msimu wa 2020/2021 ambao ilipata sita kwa vile iliishia hatua ya robo fainali hivyo ikapata pointi tatu ambazo zinazidishwa na mbili kwa vile ni msimu wa nne nyuma, kisha ina sita ilizozipata kutokana na pointi mbili ilizopata kwa kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022 ambao ni wa tatu nyuma na msimu wa 2022/2023 iliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwa vile ni msimu wa pili nyuma, zinazidishwa kwa nne kupata 12 na msimu uliopita iliishia robo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikapata pointi tatu ambazo zikizidishwa kwa tano unapata 15 na pointi hizo jumla ni 39.

Yanga imevuna pointi 32 katika misimu miwili tu ambayo ni msimu wa 2022/2023 ilipotinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikapata pointi nne ambazo zikizidishwa kwa nne kwa vile ni misimu miwili nyuma unapata pointi 16 na msimu uliopita ikapata pointi tatu kwa kuishia robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika na kwa vile ni msimu mmoja nyuma, unaizidisha kwa tano kupata pointi 15 ambazo ukijumlisha na zile 16 unapata jumla ya 31.

Chati za msimu ujao kwa maana ya 2025/2026 itatokana na mafanikio ya klabu kuanzia msimu wa 2020/2021 hadi huu wa sasa.

Kwa sasa kwa mujibu wa chati ya msimu wa 2025/2026, Simba ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 28 na Yanga iko nafasi ya 12 ikiwa na ponti 24. Yanga inaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuipiku Simba kwa vile ligi ya mabingwa Afrika ina pointi nyingi kuliko Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikiwa Yanga itaishia hatua sawa na Simba, katika msimu wa 2025/2026 itakuwa juu ya mtani wake kwenye chati za ubora za miaka mitano za Caf kwani Yanga itakuwa imekusanya pointi nyingi kuliko Simba kutokana na aina ya mashindano zinazoshiriki.

Mfano zikitokea zote zimetinga robo fainali, Yanga itakusanya pointi 39 na Simba itakuwa na pointi 38. Ili Simba iendelee kuwa juu ya Yanga, inapaswa kuhakikisha inamaliza katika hatua ya juu zaidi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kuliko ile ambayo mtani wake atamaliza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Mfano Yanga ikiishia robo fainali, Simba ili iendelee kuwa juu yao itapaswa kutinga ama nusu fainali au fainali ili ikusanye pointi nyingi ambazo hazitofikiwa na zile za yanga. Kuingia hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hakumaanishi kwamba ndio kunatosha kuifanya timu iipiku timu iliyopo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwani nayo inaweza kumaliza katika hatua za juu zaidi ya zile za mabingwa na zikakusanya pointi nyingi. 

Related Posts