Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinaunga mkono hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu kukemea vitendo vya utekaji na mauaji aliyoitoa mkoani Kilimanjaro, huku kikiwajia juu wanaoipotosha.
Jumanne Septemba 17, 2025 akifunga mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi na miaka 60 ya jeshi hilo, Rais Samia alilaani vitendo vya mauaji akisema hayakubaliki na kuagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa matukio hayo.
Pia, mkuu huyo wa nchi alisisitiza umuhimu wa wananchi kulinda amani, huku akizitaka balozi zinazowakilisha nchi zao nchini kutoingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Leo Jumamosi Septemba 21,2025 akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa wa wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema wanampongeza Rais Samia kwa hotuba hiyo, huku wakiwapinga wanaoikosoa.
“Mheshimiwa Rais (Samia) alitoa kauli ile kama Rais, kiongozi mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, lakini watu wenye nia mbaya wamekuwa wakipotosha na kuipa maana nyingine.
“Baada ya taarifa za kifo cha Kibao, Rais alitoa pole na kutoa maagizo ya kufanyika uchunguzi kwa kina, alitoa pole kwa masikitiko makubwa tofauti na wengine wanavyopotosha kauli na maagizo ya mkuu wa nchi,” amesema Makalla katika taarifa yake kwa umma.
Makalla ambaye ni mlezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam amesema akiwa ziarani Simanjiro mkoani Manyara, chama hicho kilitoa pole na kuagiza uchunguzi ufanyike kuwabaini waliohusika ili matukio hayo yasijirudie.
“Lakini cha ajabu baada ya hotuba ile ya Rais Samia kumekuwepo na upotoshaji mkubwa kwa kukata kata vipande vya hotuba hiyo kwa lengo la kupotosha umma sambamba na kutoa kauli zisizo na maana,” amesema Makalla.
Yajipanga na serikali za mitaa
Katika hatua nyingine, Makalla amesema CCM imejipanga kushinda kwa kishindo uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya na kazi nzuri iliyofanywa Serikali ya kutekeleza miradi mikubwa.
“Tumejipanga vyema hata uchaguzi ungekuwa kesho, tutashinda kwa kishindo chaguzi zote, tumeshaandaa tamko litakalotumkika katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na muda wotewote litatangazwa,” amesema.