HALI ni mbaya kwa kikosi cha KenGold ya jijini Mbeya baada ya juzi usiku kupoteza michezo wa nne mfululizo kwa kunyooshwa na Kagera Sugar mabao 2-0 ugenini, lakini kaimu kocha wa timu hiyo, Jumanne Challe ametuliza presha za mashabiki, ni upepo mbaya tu wanaowapitia, ila watakaa sawa.
Kauli ya Challe imekuja baada ya kuiongoza timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fikiri Elias kujiuzulu kutokana na vipigo vitatu mfululizo jambo linalotia mashaka mwenendo wa timu hiyo.
Kocha huyo aliyeipandisha timu hiyo kutoka Ligi ya Championship alisema ni kweli matokeo sio mazuri kwao kwa sasa, lakini bado haoni tatizo kwani ugeni na ushindani wa ligi ndiyo kinawatatiza, japo anaamini wakiizoea watabadilika.
“Sio kweli hatuna wachezaji wazuri na wazoefu wa ligi, isipokuwa ni upepo mbaya tu tumeanza nao msimu huu, inauma sana kwa sababu hatujatarajia hali hii, ila bado tuna nafasi ya kurekebisha mapungufu yaliyopo,” alisema Challe, nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania. Challe aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu msimu huu, amekabidhiwa kikosi hicho baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Fikiri Elias kuomba kuondoka mwenyewe Septemba 17, mwaka huu kwa makubaliano ya pande zote mbili kutokana na mwenendo mbovu.
“Kuna maeneo kadhaa ya kuboresha kama kwenye beki ya kati na kiungo ila kijumla tunacheza vizuri ila bahati haijakuwa upande wetu, ugeni wa ligi naona ndiyo sababu ya mwenendo huu japo sitaki kuamini ni suala la wachezaji kukosa uzoefu.”
KenGold ilianza Ligi Kuu kwa kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, ikachapwa tena 2-1 mbele ya Fountain Gate Septemba 11, ikafungwa bao 1-0 na KMC, kisha kuchapwa na ‘Wanankurunkumbi’ Kagera Sugar 2-0.
KenGold ilikuwa na mwenendo mzuri katika Ligi ya Championship ikitwaa ubingwa kwa kukusanya jumla ya pointi 70 katika michezo yake 30 iliyocheza ikishinda 21, sare saba na kupoteza miwili tu msimu mzima.