WAKATI Simba na Yanga zikiwa na mchezo wa raundi ya pili katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, kocha mkuu wa JKT Tanzania, Ahmed Ally amezipa mbinu timu hizo.
Yanga itakuwa mwenyeji wa CBE ya Ethiopia kwenye uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar, leo Jumamosi wakati watani zao, Simba watakuwa na kibarua dhidi ya Al Ahli -Tripoli kesho Jumapili kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmed alipongeza mbinu zilizotumiwa na makocha wote wawili ugenini huku Yanga ikinufaika na bao 1-0 ilhali Simba ikiambulia suluhu.
“Walimu wote walifanya mbinu nzuri ugenini, wote walipata nafasi nzuri za kupata nafasi. Kukosa kwao utulivu hasa upande wa Simba ambayo haikufunga bao hata moja bado wana faida ya kurudi kurekebisha makosa nyumbani na kutumia vyema uwanja wa nyumbani,” alisema kocha huyo wa zamani wa KMC na Tanzania Prisons.
“Safu ya ushambuliaji ya Simba inatakiwa kuongeza umakini mashindano wanayocheza yanahitaji matokeo ya ushindi ili kusonga hatua inayofuata na ni michuano ambayo nafasi huwa hazijirudii bila ya juhudi binafsi.
“Uzuri wa Simba rekodi zao uwanja wa nyumbani hazidanganyi, lakini wanatakiwa kutambua kuwa mpira ni mchezo wa makosa wakishindwa kuongeza umakini ni rahisi kwao kuadhibiwa.”
Ahmed alisema licha ya Yanga kupata faida ya bao la ugenini wanatakiwa kuongeza umakini kwa kutumia nafasi wanazotengeneza huku akikiri kuwa mpira huwa unabadilika.
“Yanga wanahitaji kuwa na njaa zaidi kuongeza umakini eneo la umaliziaji wana kikosi kizuri na kocha ambaye ni mzuri kwenye kusoma mbinu nina imani kubwa nao kuweza kusonga hatua inayofuata. Bao walilolipata lisiwafanye wakajisahau na kuamini wamemaliza mchezo bado wanatakiwa kuwa na kiu ya mafanikio zaidi ili waweze kufuzu hatua inayofuata jkwa ushindi wa mabao mengi zaidi.”
Alisema Simba na Yanga zimekuwa timu tishio Afrika licha ya kushindwa kufikia malengo makubwa ya kucheza hatua ya fainali Ligi ya Mabingwa na kutwaa kombe, lakini timu hizo zimeonyesha kupambana na kujiweka kwenye nafasi ya kushindana na timu kubwa, hivyo anaamini ni suala la muda kufikia hatua kubwa zaidi kwani kadri miaka inavyozidi kwenda zimekuwa zikiimarika.