MAMBO bado hayajawanyookea maafande wa Tanzania Prisons baada ya leo kucheza mechi ya nne mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila kupata ushindi wala kufunga bao mbele ya Dodoma Jiji.
Katika mchezo huo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa, Prisons itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi nyumbani kutokana na kutengeneza nafasi kadhaa zilizopotezwa na washambuliaji Haruna Chanongo, Vedastus Mwihambi, Zabona Mayomba na Meshack Abraham.
Prisons iliyopo chini ya Kocha Mbwana Makatta ilianza msimu kwa suluhu dhidi ya Pamba Jiji, kisha kutoka sare nyingine kama hizo na Mashujaa na Tabora United zote za ugenini kabla ya jana tena ilishindwa kupata ‘code’ ya kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wa timu hiyo.
Kwa matokeo ya jana imeifanya Prisons kutoka nafasi ya 12 hadi ya nane ikifikisha pointi nne, huku Dodoma Jiji ikichupa kwa nafasi mbili kutoka ya nane hadi ya sita kwa kufikisha pointi sita baada ya kushuka uwanjani mara tano.
Dodoma inayonolewa na kocha Mecky Maxime, licha ya kuambulia sare moja muhimu ugenini, lakini itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi kutokana na washambuliaji wa timu hiyo Wazir Junior, hassan Mwaterema na Paul Peter kukosa utulivu mbele ya lango la Prisons lililolindwa vyema na Mussa Mbisa.
Timu hizo sasa zinaenda kujiandaa kwa michezo ijayo, Dodoma ikirudi nyumbani kuikaribisha Simba Septemba 29, siku moja mara baada ya Prisons kusafiri hadi Lindi kubabiliana na Namungo.