Matampi ajichomoa mapemaa Bara | Mwanaspoti

KIPA namba moja wa Coastal Union, Ley Matampi ametangaza kujichomoa mapema katika kinyang’anyiro cha tuzo ya kipa bora kwa msimu huu, akisema haoni tumaini la kutetea tuzo hiyo aliyotwaa msimu uliopita mbele ya Diarra Djigui kutokana na udhaifu wa safu ya ulinzi ulionyeshwa katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Matampi aliyetwaa tuzo hiyo baada ya kuwa na clean sheet 19, moja zaidi na alizokuwa nazo Diarra aliyekuwa akiishikilia kwa misimu miwili mfululizo, alisema kuanza vibaya kwa Coastal sio tatizo, ishu ni namna timu inavyoruhusu mabao, jambo linalomtisha kama anaweza kurejea alichokifanya msimu uliopita.

Coastal iliyomaliza nafasi ya nne katika ligi iliyopita na kukata tiketi ya michuano ya CAF ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa raundi ya awali na Bravos do Maquis ya Angola, huku ikitinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania na kutolewa na Azam kwa kipigo cha mabao 3-0.

Timu hiyo ilianza kwa sare ya 1-1 mbele ya KMC kisha kulala 1-0 kwa Mashujaa na kucharazwa tena 2-0 na Namungo, ikiifanya katika mechi tatu isiwe na clean sheet hata moja kwani imeruhusu mabao mechi zote.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matampi aliyewahi kuwika na vigogo vya soka Afrika, TP Mazembe ya DR Congo anakotokea, alisema ni wazi wameanza msimu vibaya.

Alisema matokeo hayo ya mechi hizo tatu, japo ni mapema kuanza kuitabiri ligi, lakini inampa wasiwasi wa kama ataweza kutetea tuzo, kwani tayari amesharuhusu mabao manne katika mechi hizo kitu alichosema sio cha kawaida kulinganisha na msimu uliopita ilivyomaliza ligi kibabe.

“Mwanzo unaweza kuwa mgumu, lakini kunakupa picha ya mbele japoa sitakiwi kukata tamaa ila ubora wa makipa wengine unaonyesha ushindani wa hali ya juu. Safu ya ulinzi haijabadilika sana, lakini ikiongeza juhudi basi naweza kupata uhakika wa kutetea ushindi nilioupata msimu uliopita,” alisema Matampi ambaye kama ilivyokuwa msimu uliopita analindwa na mabeki  Jackson Shiga, Miraji Adam, Lameck Lawi na Felly Mulumba.

Related Posts