Mtoto wa Museveni ajiondoa mbio za urais 2026

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Uganda (UPDF) Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametengua nia yake ya kugombea urais mwaka 2026,  badala yake ametangaza kumuunga mkono baba yake ambaye ni Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni katika kinyanganyiro hicho.

Rais Museveni ameingoza Uganda tangu mwaka 1986 na anatajwa tena kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2026.

Machi 2023 kiongozi huyo wa jeshi nchini humo kupitia mtandao wake wa kijamii wa X alionyesha nia ya kugombea nafasi hiyo kuchuana na baba yake.

 “Mmenitaka mimi kusema daima! Sawa, kwa jina la Yesu Kristo Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na dunia na kwa jina la mageuzi bora, nitagombea urais mwaka 2026,” aliandika Jenerali Kainerugaba.

Lakini leo Septemba 21, 2024 kupitia ukurasa wake wa X, Jenerali Muhoozi ameandika kwa mara nyingine kutengua dhamira yake aliyoitangaza 2023.

“Ningependa kutangaza kwamba sitowania uongozi wa uchaguzi wa 2026, Mwenyezi Mungu ameniambia nizingatie masuala ya jeshi lake kwanza. Kwa hivyo, ninamuunga mkono kikamilifu Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi ujao,” ameandika.

Kiongozi huyo wa jeshi amekuwa akiandika taarifa zenye utata mitandaoni, ikiwemo ile aliyoandika mwaka 2022 akiwachokoza majirani zake wa Kenya, akidai jeshi la nchi hiyo lingeweza kuiteka Nairobi baada ya wiki mbili tu, huku akiwauliza wafuasi wake iwapo wangependelea aishi katika eneo la Riverside au Westland.

Siku chache kabla ya kuchapisha taarifa hiyo, pia alizua mjadala baada ya kuandika ujumbe mwingine akiuliza wafuasi wake mtandaoni ni ng’ombe wangapi Waganda wangempatia waziri mkuu mpya wa Italia kama mahari huku akiweka picha ya kiongozi huyo.

Jenerali Kainerugaba ni nani?

Jenerali Kainerugaba ni mume wa Charlotte Nankunda Kutesa aliyemuoa mwaka 1999 na pia ni mtoto wa kwanza wa Rais Museveni.

Alizaliwa Aprili 1974 mjini Dar es Salaam, akapata elimu yake ya shahada ya sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham University nchini Uingereza.

Mwaka 1999 alijiunga na UPDF akiwa ofisa kadeti na kuhitimu shahada kutoka chuo cha mafunzo ya jeshi cha Royal Military Academy Sandhurst, mwaka 2000 ambacho hutumika kwa mafunzo ya wanajeshi wa Uingereza.

Kulingana na mtandao wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Kainerugaba ni miongoni mwa wanajeshi wa Uganda waliopanda vyeo haraka haraka.

Novemba 2001 alipandishwa cheo na kuwa kapteni wa jeshi na mwaka 2002 akahudhuria mafunzo ya kuwa kamanda wa kitengo cha Jeshi (Battalion) nchini Misri.

Mwaka 2003 alipandishwa cheo cha kuwa Meja na kuteuliwa kuwa kamanda wa kitengo cha jeshi cha Motorised Infantry batallion, na mwanachama wa baraza kuu la ulinzi nchini Uganda.

Vilevile 2005 alihudhuria mafunzo ya ngazi za juu za usimamizi wa kitengo cha jeshi katika chuo cha Kaisenyi Magharibi mwa Uganda.

Mwaka uliofuata alisimamia mafunzo na mipango ya kitengo kipya cha jeshi kwa jina 1 Command katika eneo la Barlege, kaunti ya Otuke, wilayani Lira kaskazini mwa Uganda.

Julai 2008 alikuwa Mganda wa kwanza kufuzu mafunzo ya kushambulia kwa kutumia parachuti katika jeshi la Uganda la UPDF baada ya kumaliza mafunzo yake huko Marekani.

Mwaka huo huo akapandishwa cheo na kuwa Luteni kanali na kuteuliwa kuwa kamanda wa kikosi maalumu chini ya UPDF.

Septemba 2011,  akapandishwa cheo na kuwa kanali kabla ya kuwa Brigedia Jenerali.

Januari 2017, Kainerugaba aliteuliwa kuwa mshauri wa rais wa shughuli maalumu,  na  mwaka 2020 Rais Museveni akamteua tena kuwa kamanda wa kikosi maalumu (SFC) kumrithi Meja Jenerali James Birungi.

Machi 2024, Rais Museveni alifanya mabadiliko ya maofisa wa UPDF na kumteua Jenerali Kainerugaba kuwa mkuu wa jeshi hilo.

Related Posts