HISTORIA imeandikwa tena. Baada ya usiku wa jana Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo ikiing’oa CBE SA ya Ethiopia, huku Clatous Chama akiendelea kung’ara katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Yanga ikicheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, ilipata ushindi wa mabao 6-0 na kuitupa nje CBE kwa jumla ya mabao 7-0 baada ya awali kushinda ugenini bao 1-0 wiki iliyopita.
Yanga imetinga hatua hiyo ya makundi kwa rekodi ya aina yake ya kufunga jumla ya mabao 17-0 kwani katika mechi za raundi ya awali iliishinda Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.
Kocha Miguel Gamondi aliyeirejesha Yanga makundi msimu uliopita baada ya kupita miaka 25 na kwenda kung’olewa robo fainali, jana aliendeleza rekodi hiyo na kuwapa furaha Wanayanga.
Bao tamu la dakika ya 35 la Chama lililokuwa la 22 katika michuano ya CAF kwa ngazi ya klabu na lile la sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Clement Mzize liliihakikisha Yanga kuungana na vigogo kutinga makundi kabla mabao mengine manne kuongezwa ‘jioooonii’.
Katika mchezo huo, licha ya CBE kucheza soka tamu la kuibana Yanga kwa dakika 30 za awali, huku wenyeji wakipoteza nafasi nyingi, mambo yalibadilika baada ya bao hilo la Chama.
Kocha Gamondi aliwaanzishia benchi Stephane Aziz Ki, Prince Dube na Khalid Aucho na kuanza na Jonas Mkude, Clement Mzize na Mudathir Yahya, huku Yao Koaussi akirejea pia kikosini baada ya kulikosa pambano la Addis Ababa.
Pia alimchezesha Denis Nkane aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Yao, baada ya winga huyo kukosekana kwa muda mrefu uwanjani.
Mabao mengine ya Yanga jana yalifungwa na Aziz Ki dakika 75 na 90+2, huku Mudathir Yahya akitupia dakika ya 88 na Duke Abuya naye alifunga dakika ya 90+4.
Pamoja na burudani ya soka, lakini Yanga iliingia uwanjani kuonyesha imepania kuandika historia hiyo ya kutinga makundi na dakika 90 zilimalizika ikitimiza lengo.
Ushindi huo umeendeleza rekodi ya Yanga kwa msimu huu ikifikisha mechi saba na kufunga jumla ya mabao 24 na yenyewe kuruhusu bao moja tu na kuivusha Yanga makundi ikiungana na CR Belouizdad (Algeria), TP Mazembe, AS Maniema (DRC Congo), Al Ahly na Pyramids (Misri) Esperance (Tunisia) na Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates (Afrika Kusini).
Mbali na kutinga makundi, lakini Yanga imejihakikisha Sh30 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia za ‘Bao la Mama’, huku kwa kutinga makundi imejihakikisha Dola 700,000 (zaidi ya Sh 1.8 bilioni) kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo ya CAF.
YANGA: Diarra Djigui, Yao Kouassi/Denis Nkane, Chadrack Boka, DicksonJob, Ibrahim Bacca, Jonas Mkude, Maxi Nzengeli/Duke Abuya, Mudathir Yahya, Clement Mzize/Prince Dube, Clatous Chama/Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua/Stephane Aziz KI
CBE SA: Firew Alemayehu, Ephrem Dimbiso, Fetuden Jemale Ale, Caleb Amankwah, Mohamed Adem, Biruk Gebresilase, Umar Basiru, Fuad Abdu, Jima Ojulu na Suleiman Hamid
Yanga sasa inaigeukia Ligi Kuu Bara ambapo Jumatano itaifuata KenGold jijini Mbeya, huku kocha Gamondi akipiga mkwara akisema kwa sasa wao ni mwendo mdundo tu hadi kieleweke.
Kocha huyo aliyetwaa taji la ligi msimu uliopita ikiwa ni msimu wa kwanza tangu ajiunge na Yanga, aliliambia Mwanaspoti anataka kuona kila nafasi wanayoipata inageuzwa kuwa bao kwani tayari amewapa mbinu bora wachezaji.
Raia huyo wa Argentina, alibainisha kuwa mchezo wa jana dhidi ya CBE aliingia kama sehemu ya kuangalia kile alichofundisha kama kimeanza kufanya kazi, akipanga kuendeleza balaa hilo katika ligi.
Ikumbukwe katika raundi tano za ligi hadi sasa, Yanga ndiyo timu pekee iliyocheza mechi moja tu na ilianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na sasa itakuwa zamu ya kuvaana na KenGold iliyopanda daraja msimu huu..
“Naamini kwa sasa kiwango chetu cha kufunga mabao kinaendelea kuimarika, imani yangu ni tutazidi kuwa bora katika mechi zilizo mbele yetu. Malengo ni kutaka kuona kila nafasi tunaigeuza kuwa bao kwani hakuna timu inayopata ushindi bila ya kufunga mabao, wachezaji wangu wanalielewa hilo,” alisema Gamondi ambaye msimu uliopita aliifikisha Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.