SERIKALI YAHIMIZA HALMASHAURI KUIMARISHA KASI YA USIMAMIZI NA UFUATILIAJI MIRADI YA MAZINGIRA

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius (wa pili kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) ilipotembelea na kukagua Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Mafai Wilayani humo. Wa kwanza kulia ni Mtratibu wa Kitaifa wa Mradi wa LDFS, Bw. Joseph Kihaule

…..

Serikali imezitaka Halmashauri kuimarisha kasi ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya mazingira inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kuchangia katika huduma muhimu za uzalishaji kupitia ardhi, maji, misitu na bioanuai.

Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi Septemba 21, 2024 Halmashauri ya Wilaya Kondoa, Mkoani Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius wakati wa ziara ya kamati ya uongozi wa Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo Wilayani humo.

Dkt. Paul amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya mazingira na hivyo ni wajibu wa viongozi na watendaji katika ngazi za halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

“Serikali imetumia fedha nyingi katika utekelezaji wa mradi huu, nawasihi viongozi na watendaji kuendelea kusimamia kwa karibu shughuli za mradi huu ikiwemo kuzuia uingizaji wa makundi ya mifugo katika vyanzo vya maji na maeneo mengine yaliyotengwa” amesema Dkt. Paul

Aidha ameongeza kuwa mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti kasi ya   uharibifu wa mazingira hasa mmonyoko wa udongo na uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu katika halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na kuwapatia wananchi shughuli mbadala kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Ameeleza kuwa mradi wa LDFS ni mojawapo ya juhudi na jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu mazingira na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo ni wajibu kwa viongozi, watendaji na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

Nawasihi tuendelea kuwa mabalozi kwa kila mmoja wetu. Sote ni mashahidi hapa Halmashauri ya Kondoa kwani kupitia uhifadhi wa mazingira tunaona miradi ya visima vya maji imeanza kunufaisha wananchi…Hizi ni juhudi za pamoja baina yetu nawasihi tuendelee kutunza na kuhifadhi mazingira” amesema Dkt. Paul.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa LDFS, Bw. Joseph Kihaule amesema Mradi unatekelezwa katika maeneo yenye changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira hasa mmonyoko wa udongo, kupungua kwa rutuba ya udongo, uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu zilizopo katikati ya nchi na pwani.

Ameongeza kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, mradi wa LDFS unatekelezwa katika katika Kata ya Haubi (vijiji vya Haubi na Mafai) ambapo kupitia mradi huo utawezesha kuboresha mifumo ikolojia na kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kuboresha mazingira.

“Katika suala la uhifadhi wa mazingira Mradi wa LDFS umepata mafanikio makubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa hususani ujenzi wa kupendezesha makorongo katika msitu wa Intela ambao umeweza kuzuia kiasi kikubwa cha mchanga kuingia katika Ziwa Haubi” amesema Kihaule.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Haubi, Mhe. Paulo Raymond ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwezesha Kata hiyo kuwa na miradi ya uhifadhi wa mazingira ambayo imewezesha wananchi kujiongezea kipatoa na hivyo kuachana na shughuli zisizo endelevu kwa mazingira.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa hususani Kata ya Haubi kupata miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa LDFS…Tunaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha miradi hii inakuwa endelevu” amesema Mhe. Paulo.

Katika ziara hiyo kamati ya uongozi wa mradi wa LDFS ilitembelea mradi wa kituo cha kukusanya na kuhifadhi maziwa Kijiji cha Ujeji, mradi wa visima vya maji Kijiji cha Mafai, mradi wa kukusanya na kuchakata mazao ya nyuki Kijiji cha haubi, mradi wa kuhifadhi makorongo Kijiji cha Intela.

Kamati ya Uongozi wa Kitaifa ya Mradi wa LDFS inaongozwa na Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo wajumbe ni Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo.

Mradi wa LDFS unatekelezwa katika nchi 12 zilizo kusini kwa Jangwa la Sahara. Kwa Tanzania mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Kondoa (Dodoma), Nzega (Tabora), Mkalama (Singida), Magu (Mwanza), Micheweni (Pemba- Zanzibar).

Mhandisi wa Maji kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Bw. Isack Jacob (wa kwanza kulia)akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea na kukagua Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Mafai Wilayani humo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius (wa pili kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) ilipotembelea na kukagua Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Mafai Wilayani humo. Wa kwanza kulia ni Mtratibu wa Kitaifa wa Mradi wa LDFS, Bw. Joseph Kihaule

Wananchi wa Kijiji cha Mafai, Kata ya Haubi Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma wakifurahia huduma ya maji safi na salama inayopatikana Kijiji hapo ambayo imetekelezwa kupitia Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS).

Wajumbe wa kamati ya Uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) wakifurahia huduma ya maji safi na salama inayopatikana katika Kijiji cha Kiriti ambayo ni sehemu ya matunda ya utekelezaji wa mradi wa LDFS wakati wa ziara yao ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.

Afisa Misitu Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Bw. Noel Chaula (wa kwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya mtambo maalum wa kuchakata mazao ya nyuki kwa wajumbe wa kamati ya uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS) wakati walipotembelea mradi wa kituo cha kukusanya na kuchakata mazao ya nyuki kilichopo Kijiji cha Haubi, Wilayani humo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius.

Wajumbe wa kamati ya uongozi wa Mradi wa Urejeshaji wa Ardhi Iliyohabaribika na Kurejesha Usalama wa Chakula (LDFS), viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa pamoja na wananchi wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kutembelea mradi wa kuhifadhi na kupendezesha makorongo katika msitu wa Kijiji cha Intela, Haubi .

(NA MPIGAPICHA WETU)

Related Posts