Mbinga. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema mfumo wa biashara ya kahawa nchini utafanyiwa mabadiliko makubwa yanayolenga kuwanufaisha wakulima, badala ya mfumo wa sasa aliouita wa unyonyaji unaowaongezea umaskini wakulima wa zao hilo.
Amebainisha kuwa biashara isiyo rasmi ya kahawa, maarufu kama Magoma, ni haramu, na kuielekeza mamlaka wilayani Mbinga kukamata na kuitaifisha kahawa yote yaliyonunuliwa chini ya mpango huo.
Waziri Bashe ameyasema hayo Ijumaa, Septemba 20, 2024, katika Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya wizara yake.
Bashe anatembelea wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma katika utangulizi wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan inatayorajiwa kuanza Jumanne, Septemba 24, 2024.
Akizungumza na wakulima katika wilaya hiyo, Bashe amesema mabadiliko katika biashara ya kahawa yanatarajiwa kuanzisha uuzaji wa zao hilo kwa njia ya mtandao, hivyo kuwaruhusu wakulima kuona ushindani wa wanunuzi wa zao hilo kutoka maeneo mbalimbali duniani na kushiriki katika maamuzi ya uuzaji.
Amesema mabadiliko yaliyokusudiwa kuwanufaisha wakulima wa kahawa katika wilaya za Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, pamoja na wenzao wa mikoa ya Songwe na Kilimanjaro.
“Mabadiliko haya yanakuja kufuatia matokeo mazuri yaliyopatikana baada ya hatua kama hizo kuchukuliwa katika uuzaji wa kahawa mkoani Kagera na kakao inayolimwa wilayani Kyela, mkoani Mbeya,” amesema.
Amesema baada ya mabadiliko ya mfumo, bei ya kahawa mkoani Kagera ilipanda kutoka Sh7,000 kwa kilo hadi Sh12,100, wakati kakao iliuzwa kwa Shilingi 30,000 badala ya Shilingi 3,000 ya zamani.
“Biashara ya kahawa kupitia Magoma ni haramu. Wahusika wanapaswa kukamatwa na kushtakiwa kwa uhujumu uchumi. Mazao yaliyonunuliwa kwa mfumo huo yakamatwe na kupigwa mnada. Pesa itakayopatikana zituike kuzalisha miche ya kahawa itakayogawiwa bure kwa wakulima,” amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kisari Makori.
Amesisitiza kwamba miundombinu inapaswa kuandaliwa ili kuruhusu uuzaji wa kahawa kwa njia ya mtandao kupitia Soko la Bidhaa la Tanzania (TMX) litakalowezesha wakulima kuona wanunuzi wote duniani na kuwa sehemu ya maamuzi ya biashara ya mazao yao.
Bashe ameagiza vyama vya ushirika vya kahawa wilayani humo kubainisha sababu za kuomba mikopo kutoka kwenye taasisi za fesha ili kuepuka kuwatwisha mzigo wa madeni wanachama ambao hawajui matumizi ya fesha zilizokopwa.
“Vyama vya Ushirika vya Msingi (Amcos) vinapaswa kupitia rasilimali watu zao ili kuwa na uhakika wa ujuzi wa watendaji wake kuepusha vyama hivyo kuingia katika madeni yasiyolipika,” amesema.
“Mfumo wa uanachama katika Amcos unapaswa kupitiwa pia ili kuondoa ada za uanachama kwa sababu kila mtu anayejihusisha na kilimo cha kahawa anapaswa kuwa mwanachama moja kwa moja na atalipia ada zake kupitia makato yanayofanyika wakati wa mauzo ya mazao yao,” amesema.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbinga Coffee Curing, Festo Chang’a, alitaja changamoto zinazokabili maendeleo ya kampuni hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa kahawa ya kutosha kukidhi uwezo wa kiwanda hicho.
Alisema wakati kampuni hiyo ina uwezo kusindika tani 30,000 kwa mwaka, uzalishaji wa kahawa mkoani humo haujawahi kuzidi tani 25,000 kwa mwaka.
“Ukosefu wa maghala ya kutosha, pamoja na umeme wa uhakika unaoilazimisha kampuni hiyo kutumia jenereta hivyo kuiongezea gharama za uendeshaji ni changamoto nyingine zinazoikabili kampuni hiyo,” amesema.
Mbunge wa Vijana mkoani Ruvuma na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alisema matatizo ya umeme katika wilaya ya Mbinga yataisha baada ya kutekelezwa kwa mradi wa awamu ya pili wa ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme.
“Niwahakikishie wananchi kuwa kituo hicho kitajengwa mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme unaoendelea nchini,” amesema, akibainisha kuwa mahitaji ya umeme yameongezeka nchini.
Mbunge wa Mbinga Mjini, Jonas Mbunda, alisema kiwanda hicho kinachakata wastani wa tani 10,000 hadi 12,000 kwa mwaka hivyo kinafanyakazi chini ya uwezo wake halisi.
Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga, alisema minada ya kwanza ya kahawa imewapatia wakulima bei nzuri, akielezea wasiwasi wake kama bei hizo zitakuwa endelevu kwa faida ya wakulima.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Makori, alisema kikosi kazi kimefanikishwa kukamatwa kwa gunia 700 za kahawa iliyonunuliwa katika mfumo usio rasmi hivyo kuwanyima wakulima bei nzuri na mapato stahiki kwa serikali.