Simulizi kisima cha Bwibwi kilichoua maharusi na wengine 27 Dodoma

Dodoma. Kisima cha Bwibwi, kilichopo katika Kata ya Iyumbu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kina mikasa, ikiwamo ambayo hata wewe msomaji unaweza usiiamini, hasa ukiwa siyo mfuasi wa masuala ya kimila.

Hivi unajua kwa wenyewe wenye mila zao, kisima hicho hutoa sauti za filimbi, ngoma na vigelegele?

Ni kisima chenye historia ya bwana na bibi harusi wakiwa na wapambe wao 29 kufa ndani ya kisima hicho walipoingia ndani kujikinga mvua mwaka 1894 walipokuwa wakitoka harusini.

Ili kujikinga na mvua hiyo, walilazimika kuingia ndani ya kisima cha Bwibwi chenye muundo wa pango.

Walipokuwa ndani ya pango, hawakujua kuwa mvua nje ilikuwa inazidi kunyesha na kujaa kwa kasi.

Maji yalipojaakwa ghafla yakasababisha watu 29 waliokuwa wamejikinga mvua ndani ya kisima hicho kuzamishwa na maji hayo na kupoteza maisha, huku watatu pekee wakinusurika

Kisima cha Bwibwi kina sifa nyingine za kipekee ambazo zimekuwa zikisimuliwa kizazi hadi kizazi.

Ni sehemu ambayo ukoo wa Wanyanzaga katika kabila la Kigogo hufanya matambiko kila mwaka.

Imeelezwa kwamba, wakati watu walipokuwa wanapuuza kufanya matambiko, nyoka wenye sumu kali walitanda kwenye mdomo wa kisima na hivyo kuzuia watu kuchota maji na hata kudhuru wanyama wanaofugwa.

Pamoja na hayo, kuna maelezo ya kiimani kwamba sauti za filimbi, ngoma na vigelegele zilikuwa zikisikika wakati maji yanapotoka kwenye chemchemi za kisima, ikidhihirisha uhusiano wa karibu kati ya jamii hiyo na urithi wao wa asili.

Akizungumzia historia ya kisima hicho, Chifu wa Ukoo wa Wanyanzaga, Lazaro Chihoma au kwa jina maarufu Chihwelesa anasema kisima hicho kiligunduliwa na mwindaji mwaka 1872.

Chifu Chihwelesa anasema mwindaji huyo aliyeitwa Mpelembi alikuwa na mbwa wake wanawinda kwenye maeneo hayo ya Iyumbu na ndipo alipomuona ameloana maji miguuni, ikiwa ni ishara ya kupita kwenye maji na wakati huo kilikuwa ni kipindi cha kiangazi.

Anasema wakati huo mkoa wa Dodoma haukuwa na maji ya kutosha, hivyo mbwa kuloana maji ilionyesha kuwa alikuwa amepita kwenye maji mengi.

Chifu huyo anasema kesho yake alikwenda na mbwa huyo mawindoni ambapo alipopata nyama aliipaka chumvi nyingi ili mbwa huyo ashikwe na kiu na akianza kwenda kunywa maji amfuatilie kwa nyuma.

Baada ya mbwa huyo kula ile nyama alianza kwenda kunywa maji huku mwindaji huyo akiwa kwa nyuma anamfuata ili aone mahali penye maji na ndipo alipomkuta kwenye shimo ambalo lilikuwa limechimbwa na mnyama anayefahamika kwa jina la nyamhanga.

Chifu wa Ukoo wa Wanyanzaga, Lazaro Chihoma, akionyesha kisima cha Bwibwi kilichowahi kuua watu 29 wakiwamo bwana na bibi harusi.

Anasema baada ya kulichunguza vizuri shimo hilo aliona kuwa lina maji mengi, japo kilikuwa ni kipindi cha kiangazi na ndipo alipoichukua familia yake na kuhamia jirani na kisima hicho.

Anasema miaka mingi ilipita na familia ya mwindaji huyo ilikuwa ikitumia maji yanayotoka kwenye kisima hicho.

Anasema kutokana na kisima hicho kuchimbwa mara kwa mara kwa ajili ya kupata maji mengi, kilikuwa kirefu na kipana kwa ndani ambapo watu walikuwa wanatumbukia ndani kwa ajili ya kufuata maji.

Baada ya miaka mingi kupita, mmoja wa wana familia wa mwindaji huyo alienda kuoa kwenye milima ya Chihanga na walipokuwa njiani kurudi Iyumbu mvua ilianza kunyesha.

Ili maharusi wao wasiloane na maji ya mvua waliamua kuingia ndani ya kisima hicho ili kujikinga mpaka mvua itakapokatika.

Anasema kulikuwa na watu 32 walioingia ndani ya kisima hicho kwa ajili ya kujikinga na mvua na kutokana na ukubwa wa kisima hicho walikuwa hawasikii mvua ilivyokuwa ikinyesha nje.

“Kwa hiyo ili kujua kama mvua imekatika au bado walikuwa wanawatuma watu watatu kwenda kuchungulia nje kama mvua imekatika ili waendelee na safari yao,” anasema Chifu Chihwelesa.

Anasema wakati wamejificha ndani ya kisima hawakujua kuwa nje mvua iliyokuwa inanyesha iliongezeka, hali iliyosababisha maji mengi kujaa na kuanza kuingia ndani ya kisima walichokuwa wamejificha.

Chifu Chihwelesa anasema watu watatu waliotumwa kwenda kuchungulia nje ili waone kama mvua imekatika, walikutana na maji mengi.

“Na kwa sababu kisima kilikuwa kirefu walishindwa kurudi nyuma kwenda kuwataarifu wenzao watoke hivyo walionusurika katika tukio hilo walikuwa ni hao watatu tu, huku wengine 29 wakizamishwa na maji hayo mpaka leo,” anasema.

Anasema baada ya kuona hivyo wale watu watatu walikwenda kijijini kutoa taarifa za wenzao kuzama kwenye kisima, juhudi mbalimbali zilifanyika ili kuwaokoa lakini hawakufanikiwa.

Chifu Chihwelesa anasema baada ya tukio hilo kutokea watu waliendelea kutumia maji hayo kwa kuwa hawakuwa na chanzo kingine cha maji.

Chifu Chihwelesa anafafanua kuwa wakati kisima cha Bwibwi kilipolazimika kuchimbwa upya, sehemu ya kipekee ya mchakato huu ilikuwa ni milio ya sauti ambazo zilikuwa zikifuatana na ujio wa chemchemi mpya.

Kila wakati maji yalipoanza kupatikana baada ya kuchimba, eneo lilivuma na sauti za filimbi, ngoma, vigelegele na nyimbo.

Sauti hizi za kihistoria zilikuwa sehemu muhimu ya tamaduni za Wagogo, zikihusiana na sherehe na matukio ya kijamii yaliyokuwa yakifanyika wakati wa ujio wa maji.

Filimbi zilipigwa, ngoma zilitumbukizwa, na vigelegele vilipigwa kwa nguvu, huku watu wakiongozana kwa nyimbo za furaha na shukrani kwa kuwa maji yalikuwa yanapatikana.

Kwa sasa, ingawa kisima hicho kinachimbwa mara kwa mara, sauti hizi za kihistoria hazisikiki tena kwa kiwango kilekile.

Mabadiliko katika mazingira na matumizi ya kisima yameathiri hali ya sauti hizi za kihistoria.

Kwa miaka mingi, jamii imeendelea kukitumia kisima cha Bwibwi  kwa  matambiko, ambapo kila mwaka familia za watu waliopoteza ndugu zao kwenye tukio hilo hukusanyika kuwakumbuka.

Kisima hiki kimeendelea kuwa sehemu ya urithi wa kihistoria wa jamii ya Wagogo, kikiwa na hadithi za ajabu na za kuvutia kuhusu matukio yaliyowahi kutokea.

Related Posts