Dodoma. Ulevi, visasi, imani za ushirikiana na wivu wa mapenzi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mauaji ya kikatili mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Septemba 23, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema:
“Kujichukulia sheria mkononi ni kesi chache lakini sababu kubwa ni wivu wa kimapenzi, imani za kishirikina na visasi. Hayo yote yanatengenezwa na mmomonyoko wa maadili.”
Ameeleza wamewakamata watuhumiwa wanane wa makosa ya mauaji yaliyotokea mkoani humo Septemba, 2024.
Kamanda Katabazi amesema kati ya watuhumiwa hao, kesi mbili zimeshafikishwa mahakamani baada ya Ofisi ya Mashtaka kuona kuna ushahidi.
Amesema kesi tatu bado polisi wanaendelea na upelelezi.
Ameeleza suluhisho la yanayotokea ni elimu na maadili mema.
Katabazi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu akieleza wanaamini wahalifu wako ndani ya jamii.
Amesema mikakati ya jeshi hilo ni kuimarisha doria na kushirikiana na wananchi ili kupata taarifa za uhalifu na wahalifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wadau wakiwamo viongozi wa dini, wa kimila na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali.
“Tutahakikisha yeyote atakayehusika na uhalifu, tunachukua hatua kali dhidi yake kwa mujibu wa sheria. Hatutamuonea muhali,” amesema.
Kamanda Katabazi amewahakikishia wakazi wa Dodoma kuendelea kuimarisha amani na utulivu, akisema wamejipanga vizuri.
Mkakati mwingine amesema ni kuhuisha na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi na kuvipa mafunzo juu ya ukamataji salama.
Amesema kuna maeneo mengine wameshaanzisha vikundi hivyo vitakavyokuwa vinafanya doria kwa kushirikiana na wakaguzi kata.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukamatwa na noti bandia 52 na mashine moja ya kutengeneza fedha hiyo.
Amezitaja noti hizo ni za Sh10,000 zenye thamani ya Sh520,000.
Amewataja watuhumiwa kuwa Denis Mmari na Ali Muna, wakazi wa Jiji la Dodoma ambao wamekamatwa kwa nyakati tofauti Septemba 16 na 17, 2024.
Amesema jalada husika limewasilishwa Ofisi ya Mashtaka kwa hatua nyingine za kisheria.
Kamanda Katabazi amesema watuhumiwa waliokamatwa na kesi kwenda mahakamani kwa matukio yaliyojitokeza hivi karibuni ni lililotokea Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota, ambako Stephen Damas (36) alituhumiwa kumbaka hadi kumuua mwanaye kisha kumtelekeza kwa bibi yake.
Tukio jingine ambalo watuhumiwa wamefikishwa mahakamani ni lililotokea usiku wa kuamkia Septemba 6, 2024 kuhusu mauaji katika Mtaa wa Muungano A, Kata ya Mkonze ambalo Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake, Salma Ramadhan (13) waliuawa na kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Matukio ambayo bado watuhumiwa hawajakamatwa ni lililotokea usiku wa kuamkia Agosti 28, 2024 katika Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota wilayani Dodoma, ambalo Michael Richard (36) aliuawa.
Katika tukio hilo mkewe, Agnes Eliah na wanawe Ezra, Witness na Ephrahim Michael walijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Tukio lingine ni lililotokea Septemba 16, 2024 katika Mtaa wa Segu Bwawani, Kata ya Nala, ambako Milcah Robert (12), mhitimu wa darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi ya Chilohoni na mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20) waliuawa ndani ya nyumba na kisha kuchomwa moto.
Katika tukio hilo binti aliyekuwa akifanya kazi za ndani katika nyumba hiyo, Makiwa Abdallah (16) aliuawa, huku mama wa familia hiyo, Lusajo Mwasonge (40) alijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.