Wakulima wa mwani Mafia walia mabadiliko ya tabianchi

Mafia. Baadhi ya wanawake wilayani Mafia wanaojishughulisha na kilimo cha mwani na biashara ya samaki wametaja ukosefu wa elimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa masoko,  kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili kiasi cha kushindwa kujimudu kiuchumi.

Wamesema kutokana na kuwa na hali mbaya kiuchumi, kumekuwa na unyanyasaji wa jinsia kwa wanawake na watoto, wakiiomba Serikali itengeneze mazingira ya kuboresha biashara zao.

Wameyasema hayo Septemba 19, 2024 katika mkutano wa kutambulisha mpangokazi wa mradi kwa wadau wa haki za wanawake, wanaofanya kazi katika sekta ya uvuvi, kilimo cha mwani wilayani Mafia Mkoa wa Pwani.

Mradi huo wa Jahazi la ukombozi wa mwanamke wa dhidi ya ukatili wa kijinsia visiwani Mafia unatekelezwa na shirika la Mafia Awareness Centre for Government Policies (MAACEGOPO) ukifadhiliwa na Women Fund Tanzania-Trust (WFT-Trust).

Katibu wa kikundi cha wakulima wa mwani cha Nguvu kazi wilayani humo, Dora Mohamed amesema mabadiliko ya hali ya hewa yasiyotabiriwa yanawaathiri.

“Changamoto tunazokabiliana nazo ni pamoja na upepo mkali na mawimbi makali ya bahari, kwa hiyo tunahitaji elimu ya kilimo hiki, kwani wengi hatujui ni wakati gani sahihi wa kupanda zao hili. Kuna kipindi cha upepo wa Kaskazi, kuna upepo wa Kusi, kwa hiyo kuna kipindi maji yanapungua sana hivyo mwani unakuwa juani muda mrefu na hivyo kuathirika,” amesema.

Ameongeza: “Pia hatuna vifaa vya kazi kama mabuti au viatu vya chachacha na tunahitaji kamba zenye ubora ambazo pia ni gharama kuzinunua.”

Mwanachama wa kikundi hicho, Nuru Hassan amesema kwa sasa mashamba ya mwani hayako vizuri kutokana na hali mbaya ya hewa.

“Mazingira ya mashamba yetu kama yanavyoonekana hayako vizuri kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo yanatufanya tushindwe kuendelea vizuri.

“Pia tuna changamoto ya vifaa, kwa mfano hapa tunatumia tu viroba wakati wa kuvuna na tunaviburuta mpaka kwenye mwambao. Kwa hiyo tunahitaji boti itusaidie wakati wa kuvuna,” amesema.

Kwa upande wake,  Katibu wa kikundi cha Baraka Women Zaffa Bakari Selemani anasema pamoja na biashara ya samaki aliamua kuhamia kwenye kilimo cha mwani ambako pia amekutana na changamoto lukuki.

“Bado hatujawa na elimu ya kutosha ya kilimo cha mwani na pia kuna uhaba wa maeneo ya kilimo hicho, kila tunapokwenda tunaambiwa haparuhusiwi,” amesema.

Naye Zaituni Mwangia mwanachama wa kikundi hicho ameiomba Serikali kuboersha mwalo wa samaki.

“Pia kuna changamoto ya vyoo hasa kwetu wanawake ambao kuna wakati wa hedhi tunahitaji mahali pa kujihifadhi,” amesema.

Akizungumza katika utambulisho wa mradi huo, Kaimu ofisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Mafia, Maki Mbise, amesema kumekuwa na ukatili kwa wanawake wilayani humo kutokana na umasikini unaowakabili wananchi.

“Kwa hapa Mafia tushukuru kwamba tumezungukwa na bahari, vinginevyo watoto wetu wangekuwa wako Kariakoo wanaombaomba na wanafanyiwa ukatili.

“Ukatili pia unasababishwa na makazi duni, unakuta mtu ana chumba kimoja, wazazi wanalala na watoto chumba kimoja. Inawezekana una vyumba viwili, lakini watoto wa kike na kiume wanalala chumba kimoja, halafu kile chumba hakina kizuizi cha chumba kingine,” amesema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa mradi huo, Juma Kimbite amesema  umepangwa kutekelezwa kwa mwaka mmoja kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025 katika kata za Kilindoni na Ndagoni

Related Posts