Aliyekatisha masomo na kufanya kazi za ndani arejea shule

Arusha. Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Songambele, Teddy Majuto, aliyejikuta akisitisha masomo na kwenda kufanya kazi za ndani kutokana na kukosa mahitaji ya msingi ikiwemo sare za shule na madaftari, amerejeshwa shuleni kwa msaada wa wadau wa maendeleo.

Teddy ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watatu wa familia yake, wazazi wake walitengana na kusababisha kuishi maisha magumu yaliyomsababisha kukosa uangalizi wa wazazi na kukosa mahitaji hayo ya msingi.

Akizungumza jana, Septemba 21, 2024, wakati akikabidhiwa mahitaji hayo katika shule hiyo iliyopo Kijiji cha Themi ya Simba, Kata ya Bwawani, wilayani Arumeru, Teddy aliwashukuru wadau hao kwa kumwezesha kurejea shule.

Amesema mwanzoni mwa mwaka huu alijikuta njia panda baada ya kushindwa kuendelea na masomo kutokana na mgogoro wa kifamilia uliosababisha wazazi wake kuachana, hivyo kwenda kuishi na bibi yake na kushindwa kupata mahitaji hayo ya msingi.

“Niliacha shule kwa sababu kuna changamoto zilinikuta, nikaambiwa na mama kwamba baba yangu siyo Majuto, nikamfuata baba, nikamuuliza akaniambia yeye ni baba yangu, kutokana na wao kuachana sikuwa na vifaa vya shule.” “Nikamfuata baba akawa ananizungusha, nikamwambia bibi naenda kufanya kazi za ndani, zikaja mara mbili kazi za Dar es Salaam, nikakataa, ikaja ya Moshi nikakataa lakini bibi akaniambia niende, nikaenda kufanya kazi na kuacha shule.

“Kiukweli nashukuru sana kwa msaada huu, nitaweza kutimiza ndoto zangu za kusoma na kuja kuwa daktari kwani nikiwa nafanya kazi kule nikaambiwa kuna watu wananitafuta wanisaidie, nikalazimika kurudi na sasa nitaendelea na masomo,” amefafanua.

Shangazi wa mtoto huyo, Oliver Stephano amesema alilazimika kumtafuta mtoto huyo baada ya wadau wa maendeleo kutembelea shule hiyo na kuainisha wanafunzi wenye mahitaji, hivyo sasa analazimika kuishi naye ili mtoto huyo apate elimu.

“Baba yake haeleweki kila siku anasema analeta matumizi ila haleti, ameoa mke mwingine na mama yake Teddy ameolewa na mtu mwingine, hivyo nimelazimika kumchukua ili asome, tunashukuru sana kwa msaada huu,” amesema Oliver.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Agustino Migore amesema licha ya mwanafunzi huyo kuwa na uwezo mkubwa darasani, alipokumbana na changamoto hiyo aliacha shule, walijitahidi kumtafuta bila mafanikio hadi walipojulishwa anafanya kazi za ndani Moshi.

 “Tulisaidiwa na hawa ndugu zetu na amerejea shuleni na tumempokea kwa sababu elimu ni haki yake hata kama alipoteza muda mrefu tunampokea ili aweze kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zake,” amesema mkuu huyo.

Naye mmoja wa wadau hao wa maendeleo, Gillian Aron amesema alipata mguso wa kusaidia jamii hasa wanafunzi kwa kutatua changamoto za awali za kimazingira zinazosababisha wanafunzi kuwa watoro au kuacha shule kwa kukosa mahitaji ya msingi.

 “Tumeshirikiana na shangazi yake tukamrejesha mtoto na tumemletea sare za shule kwa kushirikiana na wadau wenzangu. Tuko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye ndoto anasoma ili wafikie hatima zao,” ameongeza.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Songambele, Mohamed Abdallah amewaomba wadau hao kuangalia uwezekano wa kufikia jamii hiyo kwa wingi zaidi, kwani wanafunzi wengi wana changamoto.

“Kuna wanafunzi hawana wazazi hapa na wanaishi katika mazingira magumu wanahitaji msaada, wakisaidiwa itasaidia kupunguza utoro na kuongeza morali ya kusoma,”amesema.

Related Posts