Bashe atangaza mabadiliko mfumo wa malipo wakulima wa korosho

Tunduru. Serikali imetangaza rasmi kuwa wakulima wa korosho watalipwa moja kwa moja na vyama vya ushirika badala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (Amcos) kuanzia msimu wa 2024/25.

Hayo yamesemwa Jumamosi Septemba 21, 2024 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi inayoendelea kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya wizara yake

“Kwa mfumo huu, vyama vya ushirika vitakuwa vinawalipa wakulima wa korosho mojamoja baada ya makato yote muhimu kufanyika,” aliwaambia wabunge na madiwani.

Mabadiliko hayo katika mfumo wa malipo, Waziri Bashe amesema yanakusudia kumaliza changamoto zinazowakabili wakulima wakati wa msimu wa mauzo ya korosho ikiwemo kucheleweshwa malipo na kupoteza mapato.

Malipo yatafanyika kupitia mfumo mpywa uitwao Central Payment System ambao umepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majaribio katika chama cha ushirika cha Lindi Mwambao mwaka jana.

Awali, miongozo iliwataka wanunuzi kuweka fedha kwenye vyama vya ushirika masaa kadhaa baada yam nada, kutumwa kwenye Amcos kwa ajili ya kuwalipa wakulima baada ya makato muhimu kufanyika.

Hata hivyo, katika mfumo mpya wakulima wapokea malipo yao moja kwa moja kutoka vyama vya ushirika, na kuziweka kando Amcos ambazo zilitumika kufanya malipo hayo katika mfumo wa zamani.

“Upinzani utawepo kwa sababu watu hawajazoea mabadiliko. Pili, inawezekana wapo viongozi wa Amcos waliokuwa wanatumia mfumo wa zamani kujinufaisha, hivyo hawawezi kufurahia mabadiliko haya” amesema Waziri Bashe.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi, kupitishwa kwa mfumo mpya mara nyingi kunaambatana na changamoto kadhaa kabla ya kuleta matokeo yaliyotarajiwa,” aliongeza, akirejea changamoto za awali wakati wa uanzishaji wa mfumo wa utoaji wa mbolea za ruzuku.

Zaidi, Bashe alisema serikali inafikiria kupanua mfumo huo wa malipo kwenye mazao mengine ili kushughulikia changamoto za malipo kwa wakulima nchini.

Uanzishaji wa mfumo huo ulichochea tofauti ya mtazamo miongoni mwa wabunge na madiwani wa Tunduru, huku baadhi wakiunga mkono na wengine kupinga.

Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate, alisema ana wasiwasi kuhusu hujuma, akashauri kwamba utekelezaji unaweza kuanza na mazao madogo ya kilimo kama ufuta.

“Ingawa mfumo ni mzuri, utekelezaji wake unafanywa katika wakati usio sahihi,” amesema.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu, aliunga mkono utambulisho wa mfumo huo akisema unalenga kutatua kilio cha malipo ya wakulima.

“Malipo ya wakulima wa korosho yamekuwa na matatizo kwa miaka mingi. Mkuu wa Wilaya wa zamani, Julius Mtatiro, aliwahi kuwakamata na kuwaweka rumande baadhi ya viongozi wa Amcos kwa kutumia vibaya mfumo wa malipo ya wakulima wa korosho,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Hairu Mussa, alisema mlolongo wa ufujaji fedha ni mrefu, ukianzia kwenye vyama vya ushirika.

“Kwa upande wangu, ninaunga mkono uamuzi huo kwa sababu hali ni mbaya katika wilaya hii. Mtu anaandikisha idadi ya mikorosho katika shamba lake, lakini nambari ya simu iliyoandikishwa inamilikiwa na mtu mwingine,” amesema diwani huyo wa Kata ya Mchangani.

Diwani wa Kata ya Ligoma, Abdallah Zubeir, alisema katika mfumo wa awali ilikuwa rahisi kuwafikia viongozi wa Amcos malipo yalipochelewehwa, na kuonyesha wasiswasi kama jambo hilo litakuwa rahisi katika mfumo mpya.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, alisema mfumo huo unalenga kushughulikia changamoto ambazo wakulima walikabiliana nazo katika misimu mingi iliyopita ya uuzaji koroshoa, “Sioni kama kuna tatizo katika usimamizi, wilaya yangu itasimamia kwa kikamilifu mabadiliko hayo.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Alfred Francis, alisema mwaka jana mfumo huo ulipingwa na vyama vya ushirika, akiomba ushirikiano wa wilaya kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio kwani unalenga kutoa suluhisho la malipo kwa wakulima.

Meneja Mkuu wa Tamcu, Marcelino Mrope, amesema maandalizi ya msimu wa 2024/25 unaotarajia kuanza Oktoba 29, 2024, wilayani humo umefikia asimilia 70.

Alisema Tamcu iko tayari kutumia mfumo mpya katika kuwalipa wakulima katika msimu wa 2024.24, badala ya Amcos.

“Tamcu imefanya mafunzo kuhusu mfumo mpya kwa kuwaalika viongozi wa chama cha ushirika cha Lindi Mwambao na maafisa wa ushirika toka mkoani Lindi ili kuwajengea uwezo viongozi na wasimamizi wa Amcos za Tunduru, maafisa wa ushirika na wasimamizi wa Tamcu,” amesema na kubainisha kuwa mafunzo hayo yalifanyika Ijumaa, Septemba 20, 2024.

Amesema katika msimu wa 2024/25, Tamcu inatarajia kuzalisha tani 28,000 za korosho ghafi, takriban tani 2,000 zaidi ya tani 26,062.3 zilizozalishwa katika msimu wa 2023/24.

Related Posts