Na.Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuchangia maendeleo ya elimu ya wanawake katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Ubunifu ili kuwapa fursa ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii na viwanda.
Dkt. Mahera ameyasema hayo Septemba 22, 2024 wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela (Nelson Mandela Marathon ) zilizoandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela zenye kauli mbiu ya “Jitihada kwa Sayansi, Hatua kwa Mafaniko” lengo ikiwa ni kuhamasisha wasichana na wanawake kujiendeleza na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu kwa ngazi ya Uzamili na Uzamivu.
“Kauli mbiu ya mbio hizi inashabihiana na dhamira ya Serikali yetu kupitia taasisi ya Nelson Mandela ya kukuza taaluma za Sayansi, Uhandisi, Teknolojia, na Ubunifu, ili kuwezesha kuzalisha bidhaa za uvumbuzi kwa jamii na viwanda” amesema Dkt. Mahera
Aidha Dkt. Mahera ameipongeza Taasisi ya Nelson Mandela kwa kuandaa mbio hizo zilizowashirikisha watu mbalimbali wakiwemo wenye mahitaji maalum, huku akiwataka kuwa na muendelezo kwa miaka ijayo ili kwa pamoja kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa, mbio hizo zimeandaliwa kwa mara ya kwanza kwa lengo la kukuza ushiriki mkubwa wa wanafunzi wa kike katika elimu ya juu, hasa katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu, katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Ubunifu.
” idadi ya wanafunzi wanawake katika taasisi yetu kwa ngazi ya uzamili na uzamivu ni asilimia 30 , tunatamani idadi iongezeke hata kufikia asilimia 50 ndivyo tukaona vyema kuwa na mbio hizi ili kuweka hamasa ” Anasema Prof. Kipanyula
Aidha Prof Kipanyula amewashukuru viongozi wa Serikali walioshiriki katika ufunguzi wa mbio hizo akiwemo Balozi waTanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu Makwinya kwa kushiriki mbio hizo zilizoshirikisha washiriki mia sita (600) kutoka sehemu mbalimbali nchini pamoja na nchi jirani.
Nelson Mandela Marathon 2024 ilishirikisha mbio za Km. 5, 10 na 21 huku kwa upande wa Km. 10 wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Sara Ramadhani, kwa upande wa wanaume mshindi alikuwa Faraja Lazaro ambao waliibuka na kitita cha sh. 700,000, huku washindi wa pili walipata sh.500,000 na wa tatu sh. 300,000.
Mbio za Km. 21 (nusu marathon), upande wa wanawake, ushindi wa kwanza ulienda kwa Nataria Elisanti huku kwa upande wa wanaume, Michael Gerald wakiibuka kitita cha sh. 1,000,000/= huku mshindi wa pili akiibuka n ash. 750,000 na wa tatu sh. 500,000/= .
Kwa upande wa kundi la watu wenye mahitaji maalum kwa km 21 mshindi wa kwanza alikuwa Shukuru Alfani akifuatiwa na mshindi wa pili Nasri Juma.
Wadhamini waliofanikisha mbio hizo ni pamoja Public Service Social Security Funds (PSSSF), Cocacola Bonite Bottlers Limited, Kilimanjaro Drinking Water, National Insurance Corporation (NIC), Tanzania Commission for Science and Technology (COSTECH), Ibra Line Filling Station, Beyond Experience Limited, Land Africa, Serengeti Safario Marathon, Tanzania sports Medicine Association, Tanzania Red Cross Society, Scout Tanzania, Pamoja Fitness Bonanza, Chama cha Riadha Tanzania na Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha.
Washiriki wa msimu wa kwanza wa Nelson Mandela Marathon zilizofanyika Septemba 22, 2024 wakifanya mazoezi ya utaangulizi kabla ya kuanza mbio zilizohusisha Km 5, 10 na 21 zenye kauli mbiu Jitihada kwa Sayansi, Hatua kwa Mafaniko.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera (kushoto) akivalishwa medali mara baada ya kumaliza mbio za km 10 wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Tengeru jijini Arusha.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof.Maulilio Kipanyula (kulia) akivalishwa medali mara baada ya kumaliza mbio za km 5 wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Tengeru jijini Arusha.
Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi naTeknolojia ya Nelson Mandela anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala (kushoto) Pof. Suzana Augustino akivalishwa medali mara baada ya kumaliza mbio za km 10 wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Tengeru jijini Arusha.
Washindi wa kwanza hadi wa tatu wa mbio za km 10 na km 21 wakipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera wakati wa ufunguzi wa Mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Tengeru jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera akiongea wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Lengo la mbio hizo ni kuhamasisha ushiriki wa wasichana na wanawake kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na ubunifu.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof Maulilio Kipanyula akiongea wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Lengo la mbio hizo ni kuhamasisha ushiriki wa wasichana na wanawake kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na ubunifu.
Balozi waTanzania nchini Afrika Kusini Balozi James Bwana akiongea wakati wa ufunguzi wa mbio za Nelson Mandela Septemba 22,2024 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, kushoto ni mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl Zainabu Makwinya.
Washiriki wa mbio za km 10 wakifurahia kumaliza mbio hizo wakati wa Nelson Mandela Marathon zilizoandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela zenye kauli mbiu Jitihada kwa Sayansi, Hatua kwa Mafaniko kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wasichana na wanawake kusoma masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu .