Fadlu ala kiapo Kwa Mkapa, Walibya kazi wanayo

SIMBA inatupata karata muhimu leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili itinge hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akiapa hakuna kingine cha kuthibitisha ubora wao ila kushinda na kusonga mbele.

Simba inarudiana na Walibya walioonyesha kuingiwa ubaridi mapema tangu walipokuja nchini kwa kuweka ulinzi wa mabaunsa na kukimbilia katika ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini kama kujihami pengine kwa kile kilichofanywa na mashabiki wao wiki iliyopita kuwafanyia fujo Wekundu hao baada ya kutoka suluhu.

Mchezo umepangwa kuanza mapema saa 10:00 jioni na Simba ikihitaji ushindi wowote kutinga makundi ya michuano hiyo ili kuanza msako wa kusaka taji linaloshikiliwa kwa sasa na Zamalek ya Misri.

Kinyume na matokeo ya ushindi, Simba inaweza kujikuta ikiaga mashindano hayo hasa kama mechi itaisha kwa sare yoyote ya mabao itawabeba Walibya na kama itaisha tena kwa suluhu kwa mujibu wa kanuni, mshindi itapatikana kwa mikwaju ya penalti.

Simba inasaka tiketi ya kuingia makundi katika mashindano ya klabu Afrika kwa mara ya tano mfululizo baada ya kufanya hivyo katika misimu ya 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024.

Katika Kombe la Shirikisho, Simba ilitinga makundi mara moja ambapo ni msimu wa 2021/2022 iliposhia hatua ya robo fainali ambayo ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 nma Orlando Pitares ya Afrika Kusini baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi baina yao.

Ili mpango huo wa kuitupa nje Al Ahli Tripoli ukamilike leo, Simba inapaswa kuhakikisha safu yake ya kiungo inatengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao na ile ya ushambuliaji kuzitumia vyema ili ipate ushindi ambao utaivusha kwenda hatua inayofuata.

Katika mchezo wa kwanza Simba ilitengeneza nafasi chache za mabao huku ikishindwa kuzitumia hadi kupelekea imalize mechi hiyo ikiwa haijapiga shuti hata moja lililolenga lango.

Mawinga wa Simba leo wanapaswa kuwa katika kiwango bora ili kwanza kuifanya timu itengeneza idadi kubwa ya mashambulizi kutokea pembeni jambo ambalo halikuonekana katika mchezo wa kwanza, pia ili kuwapunguza kasi mabeki wa pembeni wa Al Ahli  ambao wamekuwa silaha ya timu hiyo katika kutengeneza mashambulizi.

Katika mchezo wa kwanza, mawinga wa Simba, Joshua Mutale na Edwin Balua walionekana kupoteza mipira mara kwa mara, lakini kuna nyakati walikuwa wanachelewa kurudi nyuma kusaidia ulinzi pale timu hiyo ilipokuwa inashambuliwa jambo ambalo liliipa kazi ngumu safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Silaha kubwa ambayo Simba inaitegemea katika mechi hiyo ya leo ni safu yake ya ulinzi ambayo msimu huu imeonekana kutoruhusu kirahisi wapinzani kufumania nyavu zao.

Katika mechi tano za mashindano ambazo Simba imecheza msimu huu, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu huku mara nne ikimaliza bila kufungwa bao.

Al Ahli  yenyewe katika mechi tano zilizopita, imeruhusu bao katika mechi tatu ambapo imefungwa idadi ya mabao matatu.

Mchezo huo utachezeshwa na refa Abdoulaye Manet kutoka Guinea mwenye umri wa miaka 34.

Manet atasaidiwa na Waguinea wenzake ambao ni Sidiki Sidibe, Yamoussa Sylla na Bangaly Konate.

Huo ni mchezo wa kwanza wa mashindano ya klabu Afrika kwa Manet kuchezesha ambapo kabla ya hapo kitu pekee cha kujivunia kwa refa huyo kilikuwa ni kuwa refa wa akiba.

Ikiwa Simba itaingia makundi itajihakikishia kitita cha Dola 100,000 (272 milioni) kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Al Ahli sio timu ya kinyonge ugenini na hivyo Simba inapaswa kuwa na tahadhari kubwa katika mchezo wa leo ili kutowapa wapinzani wao fursa ya kuwaadhibu.

Katika mechi 10 za kimataifa zilizopita ambazo Al Ahli Tripoli imecheza ugenini, timu hiyo imeibuka na ushindi mara nne, kutoka sare mbili na kupoteza michezo minne.

Ardhi ya Tanzania imekuwa ni mahali pagumu kwa timu pinzani pindi zikabilianapo na Simba kwenye mashindano ya kimataifa ambapo mara nyingi zimekuwa zikipokea vichapo.

Hilo linaweza kudhihirishwa na michezo 10 iliyopita ya mashindano ya kimataifa ambayo Simba imecheza ikiwa nyumbani ambapo imeibuka na ushindi mara sita, kutoka sare mbili na kupoteza mechi mbili.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema kwa mchezo wa leo hawana kitu kingine cha kufanya zaidi ya kushinda na kufuzu makundi.

Fadlu amebainisha, watatumia mbinu zote za kimchezo kufikia malengo, huku akiwataka mashabiki kutofanya jambo la tofauti na kuwapa sapoti wachezaji wa Simba.

“Kitu kizuri ni kwamba tumefahamu namna mechi waliyotupa ugenini, malengo yetu ya kwanza yalikuwa ni kutoruhusu bao, tukafanikiwa, lakini tulihitaji kufunga ingawa haikuwa hivyo,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Kwa sasa tunapaswa kucheza kwa umakini mkubwa, tusiruhusu bao kwani tukiruhusu tunapaswa kufunga mawili ili kufikia malengo. Matarajio ni kufanya vizuri mchezo huu na kufuzu hatua ya makundi, hakuna kingine.

“Malengo ni kushinda mechi na kufuzu, kucheza nyuma ya mpira ni mbinu ya kimchezo lakini tunachokiangalia kesho ni kufuzu sio kingine. Wachezaji wanafahamu ni namna gani tunakwenda kucheza mchezo huu kutokana na tulivyofanya mazoezini.”

Kutokana na kile kilichotokea Libya baada ya vurugu kubwa zilizofanywa na wenyeji mchezo ulipomalizika, Fadlu amewataka mashabiki wa Simba kutofanya kitu cha tofauti zaidi ya kuishangilia timu yao.

“Sitarajii kuona mashabiki wakifanya kitu cha tofauti kwa wageni wetu bali natarajia mashabiki watakuwa nyuma yetu katika kutupa sapoti tunapokuwa na mpira na hata tusipokuwa nao, naamini hawatatuacha peke yetu,” alisema kocha huyo Msauzi aliyebainisha kuwa, leo atakosa huduma ya kiungo Mzamiru Yassin anayesumbuliwa na maumivu ya mguu huku matarajio yake ni kuona nyota huyo akirejea kikosini wiki ijayo.

“Mzamiru tutamkosa kwani ana maumivu ya mguu aliyoyapata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal, naamini wiki ijayo atarudi mazoezini akiwa fiti. Lakini wachezaji wengine wapo,” alisema Fadlu na kuongeza:

“Presha ya mchezo inaweza kuwepo lakini ni namna gani unaweza kukabiliana nayo, kocha unapaswa kuwasaidia wachezaji kuondokana na hiyo presha kwani tunahitaji wao kucheza vizuri. Tunafahamu kwamba matarajio makubwa sio kufuzu tu makundi bali kuchukua na ubingwa pia, hivyo lazima kuwe na presha.”

Kwa upande wa nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji alisema mchezo wa leo ni muhimu kwao na kwamba wamepata muda wa kuzungumza ili kupeana morali.

“Ukizungumzia michezo ya nyuma wachezaji wapya katika timu itakuwa wameona video na sisi huwa tunaongea wenyewe lakini kwa namna maandalizi tuliyoyafanya tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tuna deni kubwa na tunaopaswa kulilipa ni sisi, hatujafanya vizuri kwa muda mrefu kimataifa kesho ni siku ya kwenda kurudisha imani yetu kwa mashabiki, alisema Tshabalala na kuongeza:

“Hadi sasa tuna mwendelezo mzuri, mbinu anazotupatia kocha zimetufikisha hapa, kwa mechi tulizocheza taratibu vitu vinaingia kwenye timu. Mechi ya kwanza tulikuwa ugenini na kweli tulikutana na mazingira magumu, sasa tupo nyumbani hivyo mashabiki inabaki kuwa kwao kutusapoti kama wapinzani walivyofanya kwa timu yao.”

Hadi jana timu tatu za Stade Malien ya Mali, watetezi Zamalek ya Misri na RS Berkane ya Morocco iliyocheza fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita dhidi ya Wamisri ndizo zilizokuwa zimefuzu hatua ya makundi.

Jana zilichezwa mechi tatu zilizokuwa zikitoa nafasi kwa CS Sfaxien ya Tunisia, Constantine ya Algeria na CD Lunda Sul ya Angola kuungana na vigogo hivyo vya juu iwapo zingelinda matokeo ya ushindi iliyopata wiki iliyopita dhidi ya Sekhekhune ya Sauzi, Rukinzo ya Burundi na Nsoatreman ya Ghana.

Related Posts