Hii hapa asili ya utani wa makabila

Unaweza kuwa na hisia mseto unapoona watu wa kabila moja na jingine wakitoleana maneno ambayo wakati mwingine, huleta maudhi na  ghadhabu japo watu hao utaona wakifurahi,

Huo ndio hutafsiriwa kuwa utani wa jadi, ambao huruhusu watu kufanyiana dhihaka na kejeli kwa kutumia njia mbalimbali kama  nyimbo,  hadithi, misemo na hata vitendo.

Chimbuko la utani baina ya makabila limebainishwa na mtafiti,  Mahundi PD ambaye mwaka 1971  katika andiko lake: Utani Relationships: The Vidunda, anaeleza kuwa  chanzo kikuu cha utani katika makabila mengi ni biashara na vita.

Anatolea mfano makabila ya Wangoni na Wanyamwezi, Wakinga na Wasafwa, utani wao umekuwa kutokana na uhusiano wa kibiashara.

Hata hivyo, anasema kwa upande wa Wahehe na Wakinga, Wavidunda na Wangoni, chimbuko la  utani wao umetokana na vita.

Naye mtafiti,  Radcliffe-Brown aliyewahi kufanya utafiti wa masuala ya utani wa makabila kwa jamii za Afrika Mashariki, alibaini utani ni uhusiano wa kufanyiana masihara ambao ni tofauti na desturi ya kutoheshimiana.

Madhumuni yake makubwa ni kupunguza na kuondoa kabisa uhasama na chuki iliopo baina ya udugu wa makabila

Kimsingi, watafiti wamewahi kuandika kuwa utani unaweza kuchangia amani na utengamano katika jamii.

Bimize Hamad Juma katika tasnifu yake kwa ajili ya kutimiza sehemu ya masharti ya kutunukiwa shahada ya uzamili ya Kiswahili katika idara ya lugha na taaluma za fasihi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, anasema alichunguza dhima za utani wa jadi kati ya watu wa Kiuyu Minungwini na wa kisiwa cha Kojani wilaya ya Wete kaskazini Pemba.

Katika tasnifu yake alionyesha utani wa shughuli za uvuvi katika jamii hizo, kiasi kuwa wakati mwingine mtu baki anaweza kudhani utani huo utaibua uhasama mkubwa.

Anatoa mfano wa utani akiandika:

Mvuvi wa Kojani: Naona huwezi kufanya kazi mpaka uende ukapige goti “Je, nende kazini au nisende bibie.” Unamnyenyekea mkeo kama sanamu la kanisani. Hapa hatuna tu.

Mvuvi wa Kiuyu: Miye nachonga mahaba na namridhisha mke wangu si kama weye unayeridhisha vimada. Kichwa kikubwa kama cha tembo lakini akili hakina.

Huu ni mfano wa utani anaouandika Bamize katika tasnifu yake unaotumiwa na wavuvi pale ambapo mmoja wao amechelewa kufika kazini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Michezo ya Jadi kutoka Chama cha Michezo ya Jadi Tanzania,  John James anasema uko  utani wa jadi uliotokana na uhamiaji wa watu kutoka makabila tofauti tofauti.

“Ukiangalia Msumbiji unaambiwa kuna Wamakonde na huko yakazaliwa makabila mengine kama Wamakua, Wayao na Wanyasa. Mkoa wa Iringa nao yamezaliwa makabila kutokana na uhamiaji,”anasema.

Mfano mwingine anaoutolea ni kabila la Wachaga ambalo limejumuika na Wamarangu, Wakibosho, Warombo,  akisisitiza makabila mengine huzaliwa baada ya kuhama na baadayee kuleta utani baina yao na wenyeji.

“Kuna kabila linaitwa Wamwera na hawa wanatokea Lindi,  ukiangalia historia yao ni kwamba kulikuwa na mzee mmoja maarufu sana na mwenye mashamba, mzee huyu alikuwa akipeleka watu wengi kwake kwa ajili ya kulima. Kinamama wanapokwenda,  alizaa nao, sasa kwa sababu alizaa watoto wengi watu walikuwa wakimtaja sana mzee Mwera na kila mtu akawa anajitambulisha yeye ni Mmwera anapoulizwa,” anasema.

James anasema Wamwera hutaniana na Wayao kwa sababu ya ukaribu wao na wao ndio walikuwa wakifika kwa mzee Mwera kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Anasisitiza kuwa utani  ni kuambiana ukweli pasipo  mtu kukasirika sambamba  na kusaidiana.

Utani wa familia ya Kizigua na Kidigo 

Kulingana na nyaraka mbalimbali za watafiti wa lugha, mke anaweza kuwakejeli  wifi zake wanaomsifu kaka

yao kuwa anampendezesha mke wake kwa kusema:

‘’Huyo kaka yenu ajua duka la nguo lilipo

Muulize duka la nguo liwapi? Uone

kama alijua. Nguo hizi nanunua mwenyewe

Warangi hufanya utani na makabila kama vile Wahehe, wa Iringa, Wanyiramba wa Kiomboi. Ikiaminika kuwa chanzo cha utani huo ni vita baina yao.

Wahehe waliwahi kuwavamia Warangi mara mbili huku wakiteka mifugo na kuondoka nayo mara zote Warangi walipigwa.

Kwa sababu hiyo, Mhehe anaweza kumtania Mrangi kwa kumwambia: “Tuliweza kuwavamia na kuchukua mifugo yenu kwa kuwa mlikuwa dhaifu.”

Wayao na Wamakonde utani wao upo katika kunywa pombe, Wamakonde mara nyingi katika msimu wa kiangazi huwa wanafunga safari hadi kwa Wayao kwenda kunywa pombe.

Wayao wanaaminika ni mabingwa wa kutengeneza pombe. Wamakonde wakifika huko huwa wanalewa kwa haraka mno pombe hiyo.

Kwa hiyo Wayao kama wakiwa na mtu ambaye anakunywa pombe kidogo analewa mtu huyo hutafanishwa na Mmakonde.

Related Posts