Moshi. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Idrissa Makishe (38), anayedaiwa kumwagiwa kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali, amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa matibabu zaidi ya kibingwa.
Kada huyo ambaye ni mkazi wa Njoro, Manispaa ya Moshi na dereva bodaboda, alikutwa na madhila hayo usiku wa Septemba 20, 2024 baada ya mtu mmoja kumkodi akitaka ampeleke eneo la Njoro lililopo wilayani humo.
Inaelezwa kuwa baada ya kufika eneo hilo, mtu huyo aliyemkodi alimtaka asimame ampakie mwenzake ambaye alikutwa eneo la tukio akiwa amebeba chupa ya maji na nyundo, ndipo zikaanza purukushani hizo na baadaye alimwagiwa kimimimika hicho kilichomsababishia majeraha usoni na mikononi.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema wanalichunguza tukio hilo ambapo amesema baada ya watu hao kutenda tukio hilo waliondoka na pikipiki aliyokuwa anaendesha kada huyo, hivyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili watuhumiwa hao wakamatwe.
“Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa tukio la unyang’anyi wa pikipiki na kujeruhiwa kwa Idrissa Makishe (38), mkazi wa Manispaa ya Moshi, Wilaya ya Moshi baada ya kumwagiwa kimiminika kinachochunguzwa ni cha aina gani,” amesema Kamanda Maigwa.
Pia, ameongeza: “Huyu kijana alikodiwa na abiria toka kijiweni kwake ampeleke eneo la Njoro Relini, baada ya kufika eneo hilo, abiria aliyembeba alimwambia asimame ili amchukue mwenzake, ndipo alijitokeza kijana mmoja ambaye alimmwagia kimiminika hicho usoni kisha kumpora pikipiki yake.”
Akizungumzia hali ya mgonjwa huyo, Msemaji wa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, Venna Karia alikokuwa amelazwa mgonjwa huyo, amesema kwa sasa wamemhamishia hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa matibabu zaidi ya kibingwa.
“Jana jioni ilibidi tumhamishie hospitali ya KCMC kwa matibabu zaidi ya kibingwa,” ameeleza msemaji huyo wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu
Hata hivyo, tukio hilo siyo la kwanza kutokea mkoani humo ambapo mwaka 2022 lilitokea tukio linalofanana na hilo la mdau wa utalii mkoani Kilimanjaro, Tariq Awadhi, nyakati za jioni wakati akienda kutafuta chakula, alikutana na vijana wawili kwenye bodaboda na walipofika karibu yake walimmwagia kimimimika kinachosadikika kuwa ni tindikali sehemu za usoni na mikononi na kisha kutokomea kusikojulikana.