Kero sita zamsubiri Rais Samia Ruvuma

Dar/Songea. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akianza ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kesho, Jumatatu, Septemba 23, 2024, kuna masuala sita makubwa yanayowakabili wananchi wa mkoa huo ambayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwake.

Miongoni mwa masuala hayo ni kero ya ushuru wa mageti, bei ya mahindi, mbolea, madeni ya wazabuni, upatikanaji wa huduma za afya, na maji safi na salama.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Samia katika mkoa wa Ruvuma tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

Kuanzia kesho, Rais Samia atafanya ziara ya siku kadhaa ambapo atazindua na kukagua miradi ya maendeleo, na pia atazungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Wananchi wa Ruvuma wameeleza kuwa wana shauku kubwa ya kumuona Rais huyo ili kumfikishia malalamiko yao, hasa kuhusu kero ambazo hazijapata ufumbuzi wa kudumu.

Mkazi wa Peramiho-Namihoro, Castory Lupembe, ameeleza kuwa wakulima wanakabiliwa na kero ya ushuru wa mageti, hasa wale wanaosafirisha mahindi kutoka mashambani.

Amesema kuwa ushuru wa Sh 1,000 kwa kila gunia unatozwa mara mbili; unapolipia kutoka shambani na tena unapovuka wilaya nyingine, jambo linalowakera wakulima.

“Tunaomba Rais atuondolee kero hii. Mara unapolipia ushuru mahali pamoja, usilazimike kulipia tena unapovuka wilaya nyingine, maana Serikali ni moja,” alisema Lupembe.

Aziza Anderson, mkazi wa Manispaa ya Songea, ameongeza kuwa ujio wa Rais Samia utawasaidia wakulima kuongezewa bei ya mahindi kutoka Sh 700 kwa kilo hadi Sh 1,000, kwani soko la mahindi halina uhakika na bei imeporomoka sana, wakati gharama za pembejeo ziko juu.

Amesema kuwa kwa sasa bei ya mahindi mtaani ni Sh 350 kwa kilo, huku NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) ikinunua kwa Sh 700. Aziza alifafanua kuwa, licha ya NFRA kuwapo, si wakulima wote wanaoweza kuuza mahindi yao kwa sababu ya vigezo vya usafi wa mahindi vinavyowekwa na taasisi hiyo.

Kwa upande mwingine, Agnetha Focus, mkazi wa Songea, alisema kuwa wazabuni ambao hawajalipwa na Serikali wanatumaini ujio wa Rais Samia utaleta neema na kulipwa madeni yao, ambayo yamewazuia kuendesha shughuli zao za kilimo na biashara.

“Tunatarajia kupata haki yetu ya kulipwa fedha tunazodai baada ya kufanya kazi za usambazaji wa vifaa vya ujenzi na chakula,” alisema Focus.

Kadia Emmanuel, mkazi wa Mshangano, ameeleza matumaini yake kuwa ujio wa Rais Samia utasaidia kutatua kero ya huduma za afya, hasa vijijini.

 Ameeleza kuwa baadhi ya wagonjwa wanalazimika kuacha kadi zao hospitalini hadi watakapomaliza matibabu, lakini wanapoifuata kadi hiyo, wanakumbana na urasimu na kucheleweshewa kurudishiwa kadi zao, hali inayowalazimu kungoja kwa muda wa hadi wiki moja.

Wananchi wa Ruvuma wanatarajia kwamba ziara ya Rais Samia itatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto hizi zinazowakabili.

Mkazi wa Mlimani Park, Cleophanci Nditi amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, hali inayowalazimu kutumia maji ya mto ambayo hukauka wakati wa kiangazi, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa na wakati mwingine magonjwa kama homa ya matumbo huibuka.

“Naamini ziara ya Rais Samia kesho Songea itatusaidia sisi wakazi wa Mlimani Park na Namanyigu kupata suluhisho la kero ya maji safi na salama, kwani licha ya ahadi za mara kwa mara, huduma hiyo bado haijafika kwetu,” alisema Nditi.

Kuhusu mbolea, mkulima wa Liganga, Jean Komba, alisema kuwa bei ya pembejeo hiyo bado ni ya juu na haimnufaishi mkulima. Alitoa mfano kwamba ekari moja ya shamba inahitaji mifuko mitatu ya mbolea, ikiwemo ya kupandia, kukuzia na viuatilifu kwa ajili ya kuzuia wadudu waharibifu.

“Kwa bei ya sasa ya ruzuku, mbolea ya Urea ni Sh 66,500, CAN Sh 65,000, SA Sh 53,400, na DAP Sh 70,000, lakini hata bei ya mbegu za mahindi bado ni ya juu. Bei hizi ni za mijini, vijijini zinapanda maradufu. Tunaomba Rais Samia aweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha bei hizi zinapungua,” alisema Komba.

Mwenyekiti wa wakulima mkoa wa Ruvuma, Essaya Mwilamba, alisema kuwa wakulima wanakumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo kuuziwa viuatilifu feki, hali iliyosababisha hasara kwa wengi msimu uliopita na kuwaweka kwenye hali ngumu.

Mwilamba alieleza kuwa bei elekezi ya mahindi ni Sh 700 kwa kilo, lakini baadhi ya mawakala wamekuwa wakiuza kwa Sh 350 au 300 badala ya Sh 700, jambo linalowaacha wakulima bila fedha za kutosha, huku wengi wakilazimika kuuza mazao yao kutokana na dhiki. Hali hii, alisema, inaweza kuwafanya baadhi yao kushindwa kurudi shambani msimu ujao.

“Pia tunaomba mawakala wa pembejeo waongezewe fedha za usafirishaji kutoka Sh 1,500 hadi Sh 4,000 ili kusambaza mbolea kwa ufanisi vijijini, kwani Sh 1,500 ni ndogo na inaweza kusababisha foleni kubwa za wakulima kufuata mbolea mijini,” aliongeza Mwilamba.

Related Posts