Dar es Salaam. Ikiwa zimepita siku nne tangu dunia iadhimishe kumbukizi ya siku ya usalama wa wagonjwa, Zanzibar imeweka wazi magonjwa 10 yaliyoongoza kwa watu wake kutibiwa sana hospitalini kwa miaka mitatu mfululizo kati ya 2021 hadi 2023.
Magonjwa hayo yamewekwa bayana kupitia ripoti ya Zanzibar Abstract 2023 iliyochapishwa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar (OCGS) siku chache zilizopita, huku ikiutaja ugonjwa wa mfumo wa upumuaji (URTI) kuwa kinara kwa kuwa na wagonjwa wengi kwa miaka yote.
Kwa mfano kwa mwaka 2023 pekee, kati ya wagonjwa wote 1,600,238 waliotibiwa katika hospitali tofauti visiwani Zanzibar, asilimia 17.6 walikuwa ni wagonjwa URTI huku kikohozi na mafua ikiwa asilimia 13.5.
Magonjwa mengine ya ngozi yalibeba asilimia 10.6 Maambukizi ya njia ya mkojo (U.T.I) asilimia 9.7 sikio, pua na koo (8.9), kuharisha (5.2), upungufu wa damu (3.3), meno na magonjwa ya kinywa (3.1), Conjunctivitis (2.9) na ajali (2.5).
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu, magonjwa haya yamekuwa yakipishana kwa idadi ya wagonjwa jambo ambalo limekuwa likifanya yapande katika orodha ya 10 bora au kushuka kulingana na wagonjwa waliopo.
Hali hii inatajwa kuchangiwa na kutozingatiwa kwa kanuni za usafi na lishe bora, inayoweza kuujengea mwili uwezo wa kupambana na magonjwa.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Wilfred Saguda amesema huwa na sababu mbalimbali ikiwemo mtu kutokunywa maji ya kutosha ambayo ni muhimu katika kusafirisha mfumo wa mkojo.
“Sasa wengi wamekuwa hawatumii maji katika kiwango kikubwa na badala yake tunatumia vinywaji vitamu pekee, vyoo vya kuchangia kwa wanawake nayo ni sababu nyingine ya UTI, uchafu, kutozingatia kanuni za usafi, mahusiano pia yanaweza kumfanya mtu kuwa na ugonjwa huu,” amesema
Mfumo wa haja ndogo kutolindwa vyema na kuwapo kwa matumizi holela ya dawa yanayoweza kusababisha figo ishindwe kuchuja mkojo, nayo inatajwa kuwa sababu ya mtu kupata ugonjwa huo kila wakati.
Kuhusu magonjwa ya kinywa na meno amesema kutozingatiwa kwa usafi wa kinywa na mtu kushindwa kujua atumie mswaki kwa muda gani, inaweza kuwa sababu.
“Ni vyema watu wakajua watumie miswaki kwa muda baada ya hapo unatupwa, kuangalia vyakula vinavyoliwa na kuzingatia usafi wa kinywa walau kupiga mswaki mara mbili kwa siku.”
Katika hatua nyingine amesema njia hizo pia huweza kumsaidia pia mtu kuepukana na ugonjwa wa URTI ambao husababishwa ukosefu wa hewa kwenye kinywa, kutokana na uchafu jambo ambalo husababisha kuzaliwa kwa bakteria wabaya.
“Magonjwa haya pia husababishwa na zinaa ya kutumia mdomo ambayo watu wamekuwa wakiiga kutoka kwa wenzetu, pia ni vyema mtu unapokula chakula ujue ni wakati gani unapaswa kusafisha kinywa chako,” amesema.
Akizungumza namna ambavyo watu wanaweza kujikinga na magonjwa hayo, Dk Paul Masua amesema ni vyema wakaongeza uzingatiaji wa kanuni za afya bora, ikiwemo usafi wa mazingira na mwili.
“Pia kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, baadhi ya magonjwa kama ya ngozi mtu anaweza kuyapata kwa kugusana na wengine,” amesema Dk Masua.
Amesema kuchemsha maji ya kunywa ni njia nyingine ambayo mtu anaweza kuifanya ili kuua vijidudu vilivyomo ili kuepukana na magonjwa kama kuharisha.
“Kwa upande wa UTI mtu anaweza kujilinda kwa kunywa maji mengi, angalau lita 2 kwa mtu ambaye hafanyi kazi katika eneo lenye joto sana, kuzingatia kanuni za usafi ikiwemo kujisafisha kwa kina mama kwa kuanzia juu kwenda chini,” amesema Dk Masua.
Uzingatiaji wa lishe bora nalo ni jambo la muhimu ambalo mtu anaweza kulifanya ili kuujengea mwili uwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali nyemelezi na ya kuambukiza.
“Pia mazoezi ni kitu ambacho watu wanapaswa kuzingatia,” amesema.
Wakati wataalamu wakiyasema hayo, Wizara ya Afya Zanzibar, imeiambia Mwananchi kuwa inawafundisha zaidi wananchi kujikinga na magonjwa.
“Tunazo programu mbalimbali za kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa, katika magonjwa uliyoyataja hapo awali mengi yana programu zake ambazo hufanyika maeneo tofauti, wakati mwingine huambatana na kambi za madaktari bingwa ambao huwafanyia vipimo na kuwatibu wananchi,” amesema Hassan Khamis Hafidh ambaye ni Naibu Waziri wa Afya.
Amesema programu hizo pia zimekuwa zikifanya uhamasishaji juu ya watu wanavyoweza kujikinga kupitia njia mbalimbali ikiwemo runinga, redio na mitandao ya kijamii.
Anachokisema Naibu Waziri juu ya kuwafundisha wananchi kujilinda na magonjwa, huenda kikawa kimeanza kuonyesha matunda.
Hiyo ni kwa sababu, wakati magonjwa haya 10 yakiendelea kuwa mwiba kwa wananchi wa Zanzibar, takwimu zinaonyesha kuwa wagonjwa wanaofika kwa ajili ya matibabu katika hospitali na vituo mbalimbali Zanzibar imekuwa ikishuka kila mwaka tangu 2021.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, mwaka 2021 wagonjwa 2,250,609 walipatiwa matibabu katika sehemu mbalimbali za kutolea huduma idadi ambayo ilishuka hadi 1,880,226 mwaka 2022 kabla ya kufikia 1,600,238 mwaka jana.