Geita. Matukio ya ukatili wa watoto hususan ubakaji yamezidi kushamiri mkoani Geita ambapo takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha matukio hayo yameongezeka kutoka 71 mwaka 2023 hadi kufikia 91 mwaka 2024.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Tuwaambie kabla hawajaharibiwa” iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi ikilenga kutoa elimu kwa wanafunzi wanaojiunga na shule pamoja na vyuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo amesema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa iliyoathiriwa zaidi na matukio ya ukatili.
Amesema matukio hayo yanaonyesha bado ipo changamoto ya ubakaji inayoogofya ikiongozwa na imani za kishirikina kutokana na matendo hayo kufanywa na watu wa karibu.
“Tunazindua kampeni hii tukiwaambia akina mama wasiwaamini hata baba wa mtoto, unapoona baba anamshikashika mtoto maziwa, kuwa makini maana yamkini mganga wa kienyeji ameshamwambia ambake mwanaye wa miezi kadhaa, tuwe makini hali ni mbaya,” amesema Kamanda Jongo.
Mbali na ubakaji, amesema ipo changamoto ya wizi wa watoto inayosababishwa na uzembe wa wazazi, wanaotumia muda mwingi kutafuta pesa na kuacha watoto wakijilea wenyewe.
Akitaja takwimu za wizi wa watoto, Kamanda Jongo amesema kwa mwaka 2023, watoto wawili waliibiwa na kwa mwaka 2024, Januari hadi Agosti, watoto saba wameibiwa.
Kwa matukio ya mimba za utotoni, takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2023, zilikuwa 20 na mwaka 2024 zimepungua na kufikia 12 ambapo amesema kampeni ya waambie kabla hawajaharibiwa imelenga kumaliza tatizo hilo.
“Tutapita shule kwa shule kijiji kwa kijiji ili tutoe elimu kwa jamii, tuwaambie kabla hawajaharibiwa yapo matukio mengi ambayo watoto wanaharibika bila wazazi kujua hasa haya ya ubakaji, ulawiti, kuvuta bangi na ulevi na mwisho wa siku wanapotea,” amesema Kamanda Jongo.
Kuhusu matukio ya mauaji, Kamanda Jongo amesema yamepungua kutoka 89 mwaka 2023 hadi kufikia 56 mwaka 2024. Amesema yamepungua kwa sababu ya elimu inayotolewa na jeshi hilo juu ya madhara ya ukatili.
Amesema katika kampeni hiyo, Jeshi la Polisi litatoa elimu kwa watoto kuhusu madhara ya rushwa ya ngono, ukatili kwa njia ya mtandao pamoja na masuala ya uzalendo na tunu za Taifa.
Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema takwimu za matukio ya ukatili zinaonyesha bado ni tatizo kubwa na haliwezi kumalizwa na polisi na Serikali pekee, bali hilo litatimia jamii ikiunga mkono kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.
Amesema zipo sababu mbalimbali zinazochangia ukatili wa watoto ikiwemo imani za kishirikina, matumizi ya teknolojia, mabadiliko ya tabianchi yanayofanya watoto wafanye kazi ambazo ni chini ya umri wao.
“Pamoja na wazazi kuwapenda watoto na kuwapa simu au Ipad, tafakari kwa kina na kuangalia kwa jicho la ziada hiyo simu unayompa anawasiliana na nani, anaangalia nini na kwa faida gani, unaweza kuona mtoto wako yuko ndani ametulia kumbe anafanya mambo ambayo kama usingempa simu asingeyajua,” amesema Shigella.
Amesema takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2023, Januari hadi Agosti, matukio ya ukatili yaliyoripotiwa ni zaidi ya 206 na kwa mwaka 2024 kwa kipindi kama hicho matukio yaliyoripotiwa ni 104.
Ameitaka jamii kuona suala la malezi ni la pamoja na kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mtoto na kampeni ya ‘waambie kabla hawajaharibiwa’ itatoa elimu ya kuonyesha ni mazingira yapi yanasababisha ukatili na wapi pa kupeleka taarifa pindi unapoona ukitendeka.