SARE ya kufungana mabao 2-2, iliyoipata Mbeya City juzi dhidi ya Bigman FC katika mchezo wa Championship, imeonekana kuwavuruga vigogo wa timu hiyo huku kocha msaidizi, Baraka Kibingu akitoa lawama kwa mabeki na washambuliaji kikosini.
Kibingu alisema, katika mchezo huo makosa mengi yalionekana eneo la beki walioruhusu mabao mepesi na straika kushindwa kutumia nafasi walizopata ingawa wao kama benchi la ufundi wanaenda kufanya tathimini ili wasirudie yaliyotokea mwanzo.
“Tumeona makosa eneo la beki na straika, tulikuwa tushinde mchezo huu lakini umakini wetu ulipungua kwa kiasi kikubwa japo tunaenda kujisahihisha kutokana na yaliyotokea, ili mechi inayofuata tuweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Kibingu.
Kwa upande wa mshambuliaji wa timu hiyo, Mudathir Said alisema, matarajio yao kama wachezaji ilikuwa ni kushinda mchezo huo lakini haikuwa bahati yao hivyo, wanaenda kujipanga tena upya na mchezo ujao ili wasahihishe makosa yaliyojitokeza.
“Muda mwingine ni bahati tu, lakini kimsingi tumecheza vizuri na pointi moja sio mbaya, tulitarajia kuanza kwa ushindi ila haikuwezekana kutimiza hilo,” alisema nyota huyo aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo Pamba na Tanzania Prisons.