HIFADHI ya misitu ya Mkundi mkoani Morogoro itakuwa ndiyo shuhuda wa raundi ya tatu ya ubingwa wa mbio za magari kitaifa zitakazofanyika mkoani humo mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Raundi ya tatu ya ubingwa wa mbio za magari kitaifa itapigwa mkoani Morogoro tarehe 12 na 13 mwezi wa kumi kiasi cha mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa raundi ya pili mkoani Iringa.
Klabu ya Mount Uluguru ndiyo waandaaji wa mbio hizi za siku mbili ambazo kwa mujibu wa mwemyekiti wa klabu hiyo, Gwakisa Mahigi zinatarajiwa kushirikisha madereva kutoka nchini na wachache kutoka nchi za Kenya, Uganda na Zambia.
“Maandalizi yamekwisha anza na yako katika hatua za mwisho huku mazungumzo na wadhamini yakiwa pia yamefikia katika hatua nzuri,” alisema Mwenyekiti huyo wa klanu ya Mount Uluguru.
Kwa mujibu wa Mahigi, madereva wanaotarajiwa kushiriki wanatoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro,Tanga na Morogoro ambao mshiriki wake Waleed Nahdi alikuwa wa kuanza kuthibitisha ushiriki wake.
Baada ya kupata pointi 16 za kwanza katika raundi ya pili ya mbio za ubingwa wa magari kitaifa mkoani Iringa, dereva huyu chipukizi ameahidi kufanya makubwa katika raundi ya tatu ambayo amedai inachezwa nyumbani kwake.
“Nataka niwathibishie wapenzi wangu na wana Morogoro wote kwamba sasa nimekomaa kimchezo na nawaahidi kufanya makubwa katika raundi hii,” alisema Nahdi ambaye huendesha gari aina ya Subaru Impreza N10.
Raundi ya tatu inategemewa kutoa muangaza wa nani anastahili kuutwaa ubingwa wa mbio za magari kitaifa kati ya madereva kutoka Dar es Salaam na wale kutoka Arusha.
Kuelekea mbio za raundi ya tatu, Manveer Birdi wa Dar es Salaam ndiye anayeongoza kwa pointi akifuatiwa na Gurpal Sandhu wa Arusha na Randeep Birdi wa Dar es Salaam.
“Naamini nitaurudia tena uongozi baada ya kushindwa kumaliza mbio za magari za Iringa kutokana na gari yangu kupata hitilafu katika hatua za mwishoni kabisa,” alisema Randeep Birdi ambaye aliukwaa uongozi baada ya kushinda raundi ya kwanza mjini Tanga.
Kuna raundi tano mwaka huu ili kukamalisha kalenda ya mbio za magari kwa msimu huu.