Mbwana Makata akiri mambo magumu

WAKATI mashabiki wa Prisons wakishangazwa na matokeo ya sare nne mfululizo, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata amesema ligi ni ngumu na haina cha nyumbani na wala ugenini, huku akipongeza mabeki wake.

Prisons imeanza kwa ugumu Ligi Kuu baada ya kufululiza sare nne bila kupata bao wala ushindi na kuwaamsha mashabiki wakieleza matokeo si mazuri sana na inahitaji juhudi za ziada.

Mafande hao walianzia mechi tatu ugenini wakiambulia suluhu dhidi ya Pamba Jiji, Tabora United na Mashujaa na jana wakiwa Sokoine jijini Mbeya waliendeleza matokeo hayo mbele ya Dodoma Jiji.

Timothy Mwampashi shabiki wa timu hiyo, alisema licha ya wachezaji kucheza vizuri lakini bado kuna uhitaji wa nguvu za ziada kuondokana na mzimu wa sare na kujiweka pazuri kwenye msimamo.

“Tulisema timu imeanzia ugenini sare siyo mbaya, lakini leo tena dhidi ya Dodoma Jiji yanatokea yaleyale hapa Sokoine, lazima vijana wapambane tuondoke huku kwani mechi zinasogea hakuna cha kusubiri,” alisema Mwampashi.

Akizungumzia matokeo hayo, Makata alisema ligi imekuwa ngumu lakini kinachowapa matumaini ni kuwa hawajapoteza mchezo wowote.

Alisema pamoja na kutofunga bao katika mechi zote, lakini pia hawajaruhusu bao wala kupoteza na kwamba benchi la ufundi linaenda kufanyia kazi makosa ili mchezo ujao dhidi ya Namungo waweze kushinda.

“Ligi ni ngumu, kila timu imejiandaa na hakuna cha ugenini wala nyumbani, popote unaweza kupata matokeo kutegemea na mipango na maandalizi binafsi, tumeona penye tatizo tutafanyia kazi.

“Mabeki wamefanya kazi nzuri kwakuwa hatujaruhusu bao ni ile tu kukosa bahati kwa mastraika kufunga mabao, tutajipanga upya kwa ajili ya mechi ijayo dhidi ya Namungo ili tushinde na kujiweka pazuri,” alisema kocha huyo.

Related Posts