Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watakaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri nchini.
Amewataja maofisa maendeleo ya jamii, wasimamizi wa fedha, waratibu wa mikopo, wahasibu na maofisa Tehama wa mikoa na wilaya ambao watabainika kujihusisha na ubadhirifu wa fedha hizo za mikopo kuwa atawachukulia hatua.
Mchengerwa alibainisha hayo jana Jumamosi, Septemba 22, 2024 jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya wasimamizi wa mikopo hiyo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zote nchini.
“Mikopo hii inatolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali, hivyo sitosita kuwachukulia hatua watakaokwamisha makundi lengwa kupata mikopo,” alisisitiza.
Ikumbukwe awali, Serikali ilisitisha mikopo hiyo kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Aprili 13, 2023 wakati akihitimisha hoja ya makadirio ya maombi na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24.
Uamuzi wa kusitishwa kwa mikopo hiyo ulitangazwa ili kupisha utaratibu mwingine wa utoaji kutokana na malalamiko ya namna zinavyokopeshwa na urejeshaji, ikiwemo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Hata hivyo, Aprili 16, 2024, Waziri Mchengerwa alitangaza kurejeshwa kwa mikopo hiyo wakati akisoma bajeti yake ya mwaka 2024/25.
Alisema halmashauri 10 za majaribio zitaanza utoaji kwa kutumia benki ambapo mikopo inayotarajiwa kutolewa ni Sh227.96 bilioni ambapo Sh63.67 bilioni ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa.
Sh63.24 bilioni ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na Sh101.05 bilioni ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25.
Alizitaja halmashauri 10 zitakazoanza kutoa mikopo hiyo ni ya Jiji la Dar es Salaam, Dodoma, Songea, Kigoma Ujiji, Mbulu, Newala Halmashauri ya Wilaya ya Kitilima, Nkasi, Bumbuli na Siha.
Alisema halmashauri 174 zitapata mikopo kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan fedha hizo ziwafikie walengwa.