Dar es Salaam. Umedumu kwa muda gani kwenye ndoa au uhusiano wako? Katika maisha yote umewahi kuchepuka? Nini kilisababisha ufanye hivyo?
Maswali hayo yanagusa sehemu ya tabia za wanaume wengi walio kwenye ndoa au mahusiano yaliyodumu, ambao aghalabu hujikuta wakishiriki mapenzi na wenza wa ziada ‘michepuko.’
Hali hiyo, inawafanya baadhi yao kujikuta wakishindwa kuchomoka katika penzi la michepuko na hatimaye wanasahau familia au wenza wao halisi na halali.
Ingawa kuchepuka kunafanywa na wanawake pia, lakini wanaume wanatajwa kuwa vinara kwa vitendo hivyo, kama wanavyolalamikiwa na wenza wao.
Mariam Tabuya anasema kwa sasa anaishi mwenyewe baada ya kutengana na mwenza wake na michepuko ndiyo sababu ya hali hiyo.
Anaeleza halikuwa kusudi lake kuishi mwenyewe, bali mwanamume wake huyo aliyemuoa kwa ndoa halali ya Kiislamu, alihama nyumba na kwenda kuishi na mchepuko.
“Alianza taratibu, nikawa naona tabia zinabadilika, mara akawa anapokea simu kwa siri, ukafika wakati simu yake ilikuwa inafichwa, nikaja kubaini ana simu mpya anaitumia akiwa kazini, hatimaye akahama na nyumbani kabisa,” anasema.
Kwa mtazamo wa Mariam, hakuna sababu nyingine ya mwanamume kuchepuka zaidi ya tabia binafsi, ambazo huwa nazo tangu anapoingia rika balehe.
Anaeleza udhaifu wa mwanamke na sababu nyingine, haziwezi kumfanya mwanaume achepuke, akisisitiza ingekuwa hivyo kila mume angeshachepuka.
“Kwa sababu hakuna binadamu aliyekamilika, sasa ukichepuka kwenye kila udhaifu wa mwenzio si utachepuka na dunia nzima. Wasitafute sababu, anayechepuka ni tabia yake,” anasema.
Mke na mama wa watoto wawili anayeishi Dar es Salaam, Bernadetha Luanda anasema wametengana na mwenza wake baada ya kumfumania akichepuka katika nyumba waliyokuwa wanaishi.
“Nilisafiri kwa ajili ya uzazi, nikapewa taarifa kuwa kuna mwanamke mwenzangu nyumbani, nikarudi bila kumtaarifu, niliwakuta ndani, tukatengana kuanzia hapo,” anasimulia.
Bernadetha anasema tamaa za kimwili ndizo zinazowasababisha wanaume wachepuke.
Anaeleza hakuna kipya anachokutana nacho mchepukaji, zaidi ya kilekile alichokianza kwa mwenza wake halali, lakini tamaa inawafanya wajaribu huku na kule.
“Hakuna lolote, ni tamaa zimewajaa, hata ufanye vipi hawa watu wameumbwa na tamaa na watachepuka tu. Muhimu ni kuishi nao ukitambua kuwa watachepuka ili usiumize kichwa,” anaeleza.
Salma Msangi anasema mwanamume kuwa na mwanamke zaidi ya mmoja ni maumbile kutoka kwa Mungu, ndiyo maana dini ya Kiislamu imewaruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja.
“Wameumbwa hivyo, ndiyo maana Mungu ameona muhimu awaruhusu waoe wanawake wanne. Mimi sipendezwi na wanaume kuchepuka, lakini hilo tulitarajie,” anaeleza, huku akikiri kuwahi kuona mazingira yanayoashiria mwenza wake kuchepuka.
Mkazi wa Dar es Salaam, Meshack Abraham anasema wakati mwingine wanajikuta wakichepuka siyo kwa kukusudia, bali ni uhalisia wa vituko na vishawishi vilivyopo kwa wanawake.
“Unakuta mtu huna nia naye kabisa, lakini maumbile yake na mavazi anayovaa, zaidi ni namna anavyojirahisisha, unajikuta umeshawishika kuchepuka,” anaeleza.
Hilo ni tofauti na Yusuph Mussa (si jina halisi) anayesema anachepuka kutafuta ladha mpya, baada ya kuzoea anayoipata kwa mwenza wake rasmi.
Mussa, anayefanya kazi ya udereva wa taksi mtandao, anaeleza mwanamume ameumbwa kutamani kitu kipya kila anapokutana nacho, ndiyo maana hata wachepukaji hawana mchepuko mmoja.
“Tumeumbwa kujaribu ladha mbalimbali, leo ukimpata huyu mwenye maumbile haya unatamani mwenye maumbile yale atakuwaje, hapo ndipo tunajikuta tuna mnyororo wa wanawake wengi,” anaeleza.
Kwa mtazamo wa Bahati Msami, mwanamume kuchepuka kunachochewa na uhalisia wa kibaiolojia alionao, ameumbwa kutoridhika, hivyo furaha yake ni kuwa na wengi.
Lakini, Deus Deus anasema aliwahi kuchepuka baada ya maelewano duni na mkewe, hata hivyo ilisaidia kukomesha tabia mbaya aliyokuwa nayo mwenza wake huyo.
“Kweli alinifumania na ukawa ugomvi mkubwa, lakini nilimweleza ukweli kwanini nimefanya hivyo akajirekebisha. Naona imenisaidia, siwashauri watu watumie silaha hiyo kuwarekebisha wenza wao, lakini mimi ilinisaidia,” anasema.
Uamuzi wa mwanaume kuchepuka, unasababishwa na kuitafuta furaha au faraja ambayo aghalabu kwa mwenza wake halali anaikosa, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mgolanga Shagembe.
Mwanazuoni huyo anasema ingawa wengi hudhani kuchepuka ni tabia ya mtu, kiuhalisia inachochewa na kusaka jambo analolikosa kwa anayepaswa kumpatia bila kujali ni jambo jema au baya.
Anasema hali inakuwa mbaya zaidi, pale mchepukaji anapoeleza udhaifu wa mwenza wake kwa mchepuko.
Hali hiyo kwa mujibu wa Dk Shagembe, inamfanya mchepuko atumie udhaifu wa mwenza halisi kama silaha ya kumshawishi zaidi mwanamume huyo.
“Unakuta mchepuko anamtimizia yote ambayo alikuwa anayakosa kwa mkewe, atafanya hata kwa kuigiza kwa sababu ana maslahi anayoyatarajia kwa mwanamume huyo,” anasema.
Katika mazingira hayo, anaeleza mwanamume atatoa kila hitaji la mchepuko na wakati mwingine hata kufikia hatua ya kumpunja mkewe au kumsahau kabisa.
Mwanazuoni huyo anasisitiza, hali hiyo ndiyo inayomfanya mwanamume anaonekana kumng’ang’ania mchepuko hata anapofumaniwa au kukemewa na yeyote.
“Analazimika kufanya hivyo kwa sababu moyo wake unaanza kupata furaha ambayo aliikosa kwa mkewe na hapo ndipo anapojikuta haelewi lolote wala chochote,” anasema.
Kinachomfanya mwanamke asimtimizie mwenza wake, anasema ni kukosa stadi za maisha zinazomfanya asiwe na uwezo wa kuonyesha hisia zake, kuzungumza na hata kukabiliana na changamoto.
Anasema mambo hayo yanamfanya mwanamke ama awe mkorofi baada ya ugomvi na mwenza wake, au asionyeshe hisia zake kwa mwenza.
Yote hayo, Dk Shagembe anasema yanasababishwa na ombwe la mafunzo na uchunguzi stahiki, kabla ya wenza kuamua kufunga ndoa.
Anasema watu wanadhani kupima Ukimwi ndilo hitaji pekee la msingi kabla ya kuingia kwende ndoa, ilhali kunahitajika vipimo vingine kama vya akili na uwezo wa kuhusiana na wengine.
“Kuna mtu katika maisha yake hana uwezo wa kuhusiana na wengine, ukiingia naye kwenye mahusiano ni tatizo. Lakini hata mwenye shida ya afya ya akili ni tatizo pia kwa sababu anakosa uwezo wa kutatua changamoto,” anaeleza.
Anaeleza wenza wengi hawafahamu kwamba inapotokea changamoto haipaswi kuachwa imalize siku, inapoachwa inazidi kuwasogeza mbali wenza kihisia.