Mufti atoa rai ya kuheshimiana, Kunenge akemea siasa kwenye nyumba za ibada

Kibaha. Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi amesisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimiana kama njia ya kudumisha amani nchini.

Muft  alisema hayo usiku wa jana Jumamosi, Septemba 21, 2024 katika sherehe za Maulidi zilizofanyika mjini Kibaha, zilizoandaliwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Pwani.

Alisema ukosefu wa heshima miongoni mwa watu ni chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani.

“Mdogo ana wajibu wa kumuheshimu mkubwa na mkubwa ana wajibu wa kumuhurumia mdogo. Hapo hakutakuwa na fujo wala mvutano,” amesema.

Aidha, ameweka wazi baadhi ya tabia zinazoshuhudiwa katika jamii, kama vile kutukana viongozi bila sababu ni dalili ya kukosekana kwa maadili mema.

“Kiongozi yoyote lazima aheshimiwe na ni wajibu wa kila mmoja kutunza maadili katika jamii,” ameongeza.

Pia, amekemea vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza ni muhimu kuripoti makosa kwa mamlaka husika badala ya kuchukua hatua za kulipiza kisasi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani (RC), Abubakari Kunenge amesema matumizi ya nyumba za ibada katika siasa yanapaswa kupigwa vita, kwani yanachangia mvurugano katika jamii.

“Ni muhimu viongozi wa dini wajiepushe na siasa ili tuendelee kutangaza maneno ya kiroho,” amesema.

Kunenge amehimiza wazazi kuimarisha malezi ya watoto wao ili kukemea vitendo viovu, akirejelea ongezeko la maadili yasiyofaa kwenye jamii.

“Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na hali hii ambayo ni hatari kwa jamii,” amesema

Kwa upande wake, Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa amewataka waumini kudumisha amani iliyopo ili kulinda usalama wa watu na mali zao.

“Amani ni muhimu katika kila nyanja ya maisha yetu, bila amani hatuwezi kufanya kazi zetu,” amesema.

Related Posts