KIPA mpya wa Fountain Gate Mnigeria, John Noble amesema licha ya kutocheza mchezo wowote wa Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho kilichomsajili msimu huu kutoka Tabora United, bado hana wasiwasi na nafasi yake kikosini, huku akisifu kiwango bora kinachoonyeshwa na kipa mwenzake, Fikirini Bakari.
Noble aliyejiunga na Fountain Gate msimu huu akitokea Tabora United, ameshindwa kuichezea timu hiyo kutokana na kutopata vibali vya kufanyia kazi nchini jambo lililomfanya akose michezo mitano ya Ligi Kuu Bara hadi sasa ya kikosi hicho.
“Inauma ila bado michezo iliyobaki ni mingi na naamini nitakapoanza kucheza nitafanya vizuri kama ambavyo mashabiki zetu wanatarajia, naheshimu kiwango bora cha Fikirini Bakari kwa sababu ni kipa mzuri anayenipa changamoto mpya,” alisema Noble.
Akizungumzia malengo yake msimu huu Noble alisema, lengo lake kubwa ni kuvuka rekodi ya kutoruhusu mabao ‘Clean Sheets’ aliyoiweka msimu uliopita na alikuwa na 13 katika michezo 22 ya Ligi Kuu Bara aliyocheza na Tabora United.
“Kama mchezaji ni vizuri kujifanyia tathimini ya kile ulichokifanya msimu uliopita na huu wa sasa, ili kufikia malengo hayo ni lazima nipambane zaidi kwa sababu nimekosa michezo mitano ya mwanzo jambo linalozidi kunipa ugumu huo,” alisema.
Kwa mara ya kwanza kipa huyo alitua nchini Julai 31, mwaka jana na kujiunga na Tabora United akitokea Enyimba ya kwao Nigeria na mechi alizozikosa msimu huu ni ule wa juzi dhidi ya chama lake la zamani, Tabora United waliyoifunga mabao 3-1, ile ya kipigo cha 4-0 kutoka kwa Simba na nyingine mbili za ugenini za ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo na 2-1 dhidi ya KenGold na sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji na kuifanya ikusanye pointi 10 ikishika nafasi ya pili nyuma ya Singida BS yenye alama 12.