Saa 72 Kigoma zilivyowaacha watano wakihukumiwa kunyogwa

Kigoma. Zilikuwa ni saa 72 za moto, ndivyo unavyoweza kuelezea hukumu sita za mauaji zilizotolewa na Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu mjini Kigoma huku watu watano wakihukumiwa adhabu ya kifo na mmoja miaka 10 jela.

Hukumu hizo zilizotolewa kati ya Septemba 18 na 20, 2024 na kuongeza idadi ya watu waliohukumiwa kunyongwa hapa Tanzania kuwa zaidi ya watu 700, baadhi wakisubiri kunyongwa na wengine wakiwa hatua mbalimbali za rufaa.

Kwa sheria za Tanzania, mahakama ya Rufani ndicho chombo cha mwisho cha rufaa kwa mashauri ya mauaji na Tanzania haijawahi kutekeleza adhabu ya kifo kwa miaka 29 sasa na hadi Mei 2023, waliohukumiwa kunyongwa walikuwa 691.

Hata hivyo, tangu takwimu hizo zitolewe Mei 2023, idadi ya waliohukumiwa kunyongwa inatajwa kuongezeka na si chini ya watu 10 wameingia katika orodha ya waliohukumiwa adhabu ya kifo na mahakama katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa wale waliofika mwisho katika hatua ya rufaa, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee, ndiye mwenye mamlaka ya kusamehe na kumwachia huru mtu aliyepatikana na kosa lolote liwe au kupunguza adhabu.

Hukumu za kifo mkoani Kigoma

Mojawapo ya hukumu hizo ni ya wanawake wawili kuhukumiwa kifo, mmojawao ni ndugu wa damu na ndiye aliyekodi muuaji kwa gharama ya Sh70,000 ili kumwekea sumu dada yake, Amina Bazila na akalipwa malipo ya awali Sh20,000.

Katika simulizi hiyo, mshitakiwa wa pili, Evodia Bazila, alimkodi mshitakiwa wa kwanza, Aneth Tabu ambaye ni rafiki wa karibu na marehemu na kumpa ugoro ambao umechanganywa na sumu na akampa ‘besti’ yake huyo na kumuua.

Makubaliano yalikuwa ni kwamba Aneth alilipwa malipo ya awali ya Sh20,000 kati ya Sh70,000 walizokuwa wamekubaliana, ambapo siku ya tukio hilo Mei 5,2022 huko mkoani Kigoma, Aneth akampa rafiki yake huyo sumu.

Hukumu ya adhabu ya kifo imetolewa Septemba 19, 2024 na Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ambaye alisema adhabu kwa kosa la mtu anayetiwa hatiani kwa kuua kwa kusudia ni moja, nayo ni kunyongwa hadi kufa.

Katika kesi hii ya Jamhuri dhidi ya Miburo Mussa, hukumu yake ilitolewa ilitolewa Septemba 20, 2024 ambapo Miburo alishitakiwa kwa mauaji ya Nemeimana Jacqueline, mauaji yaliyotokea Agosti 17, 2020 huko katika wilaya ya Kibondo.

Marehemu alifariki dunia baada ya kupata majeraha mabaya ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani, kwenye bega na kiganja ambapo vidole vilikatika kabisa na mashuhuda walishuhudia mshitakiwa akimshambulia marehemu kwa panga.

Kiini ni kinyongo dhidi ya marehemu ambaye alikuwa ameolewa na mshitakiwa kabla ya marehemu kumpora na kumuoa jambo lililoibua chuki na visasi.

Shahidi wa tano na mashahidi wengine walimkamata akiwa bado ameshikilia panga alilolitumia kufanya mauaji hayo lakini katika utetezi wake, mshitakiwa alionyesha kushangazwa kushitakiwa kwa mauaji hayo ya kukusudia.

Aljitetea akisema siku ya tukio hakuwa ametumia hata dakika moja nyumbani kwake wala karibu na eneo la tukio kwani siku nzima alikuwa akijenga nyumba ya mkimbizi mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au DRC.

Alieleza kuwa baada ya kumaliza kujenga alikwenda moja kwa moja msikitini.

Katika hukumu yake, Jaji alisema kuna ushahidi wa wazi kutoka kwa mashahidi wa Jamhuri kuwa walimuona mshitakiwa akimshambulia marehemu kwa panga.

“Nakubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa alikamatwa eneo la tukio na utetezi wake kuwa siku ya tukio alikuwa akijenga nyumba ni uongo na aliutoa ili kujinasua tu na kosa hilo,” alisema Jaji Nkwabi katika hukumu yake.

Sh3,000 zilivyosababisha mauaji

Kaika kesi hiyo ya Jamhuri dhidi ya Sudy Omary au Sudi Mawela hukumu yake, ilitolewa Septemba 2024 ambapo mauaji hayo yanadaiwa kutokea Mei 21,2023 katika Kijiji cha Kumwambu katika wilaya ya Kibondo katika mkoa wa Kigoma.

Mwanamke aitwaye Ashura alimpoteza mume wake na ushahidi wa Jamhuri ulionyesha kuwa kifo cha Joseph Misigaro kilisababishwa na mshitakiwa aliyempiga makofi mawili na kufanya fuvu lake kuvunjika na ubongo kutikisika.

Hiyo ilisababisha damu kuganda na kusababisha uvimbe kichwani na kusababisha kifo chake ambapo mshitakiwa alikamatwa akiwa eneo la tukio.

Wananchi waliofika eneo la tukio walimchukua majeruhi wakati huo pamoja na mshitakiwa na kuwapeleka polisi ambapo majeruhi alipatiwa fomu ya polisi namba tatu (PF3) kwa ajili ya matibabu na mshitakiwa akaendelea kuhojiwa.

Marehemu alifariki Mei 22,2023 mbele ya mtoto wake wa kiume na kulingana na ushahidi, kiini cha mauaji hayo ni kutokana na mkewe kulipwa Sh3,000 na mshitakiwa kwa ajili ya kuvuna mahindi lakini hakwenda kuvuna kwa wakati.

Mshitakiwa alikwenda kuhoji kulikoni ambapo marehemu alimweleza kuwa mkewe angeifanya kazi hiyo Jumatatu, jibu halikumridhisha na ndipo akamzaba vibao viwili ambavyo vilimfanya marehemu kuanguka sakafuni na kuzimia.

Jitihada za kuokoa maisha ya marehemu hospitalini hazikuweza kuzaa matunda.

Mshitakiwa alikuwa anakanusha shitaka hilo na kudai siku hiyo akiwa anatokea kuchimba mawe, alikutana na watoto wawili wa marehemu ambao walimpeleka hadi eneo la tukio ambako marehemu alikuwa amelala chini amepoteza fahamu.

Aashangaa kushitakiwa kwa mauaji lakini Jaji katika hukumu yake akasema ingawa alijitetea kuwa alikuwa ameenda kuchimba mawe umbali wa mita140, umbali huo hautoshi kusema asingeweza kufanya mauaji hayo.

Lakini pia akaegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza aliyemuona akimzaba vibao mumewe na ndiye aliyepiga ukunga na mashuhuda wengine kufika eneo la tukio.

Wivu wa mapenzi ulivyotoa roho

Kesi hii ilikuwa ni baina ya Jamhuri dhidi ya Edward Basesegwa na hukumu yake ilitolewa Septemba 19, 2024 kutokana na mauaji ya Helena Nzeluke aliyewahin kuwa mke wa mshitakiwa na inaelezwa kinyongo cha kuachana kilikuwa kiini.

Usiku wa Oktoba 16, 2022, marehemu alishambuliwa hadi kufa akiwa katika chumba alichokuwa amepanga wakati huo watoto wake wa kiume walikuwa wameenda eneo la kibiashara kijijini hapo kwa ajili ya kuvinjari.

Wakiwa njiani wanarudi, walikutana na mshitakiwa akitokea katika nyumba ya mama yao na ilionekana walipokutana hawakusemeshana kwa vile mshitakiwa alikuwa haishi tena ana mama yao, lakini akawarushia nyundo na kukimbia.

Hiyo iliwafanya washuku jambo na walikimbilia nyumbani kwa mama yao na kumkuta amelala katika dimbiwi la damu akitokwa na damu nyingi kichwani akiwa amepoteza fahamu, alipelekwa hospitalini Kibondo lakini alifariki dunia.

Katika utetezi wake, mshitakiwa alidai kuwa muda wa tukio hilo alikuwa akiishi tofauti na marehemu na kwamba mrehemu alikuwa akiishi Gwanumpu center Jirani na kituo cha Polisi na yeye alikuwa akiishi mbali kidogo na marehemu.

Alikanusha kugombana na marehemu na kwamba ni mmoja wa watoto wake ndiye aliyemshawishi mama yao kuachana naye na kusema asingeweza kumuua marehemu kwa kuwa hakuwa amempa talaka hivyo hakuwa na ugomvi naye.

Utetezi huo ulikataliwa kutokana na kuwepo kwa muungano wa ushahidi uliotolewa na watoto na mashahidi wengine ambapo Jaji Nkwabi alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo na kumwambia anayo haki ya kukata rufaa.

Alivyotupwa jela miaka 10 kwa mauaji

Katika kesi hiyo, Jamhuri ilimshitaki Rosemary Majaliwa kwa mauaji ya bila kukusudia na hukumu yake ilitolewa Septemba 18, 2024 na Jaji Nkwabi.

Mawazo Faida alifariki Agosti 13, 2023 katika kitongoji cha Kumgarika huko wilaya ya Kibondo na kulingana na ushahidi, usiku wa Agosti 12, 2024, kulizuka ugomvi kati ya mshitakiwa na marehemu na walishambuliana kwa kurushiana mawe.

Moja kati ya mawe hayo lilimpata Mawazo tumboni, akaenda kulalamika kwa dada yake juu ya kupata maumivu ya tumbo na siku iliyofuata alipelewa hospitali kwa ajili ya matibabu na baadae alifariki dunia.

Uchunguzi wa daktari ulibaini sababu ya kifo ni kupata majeraha ya ndani ya mwili yaliyosababisha kupasuka kwa wengu. Mshitakiwa alijitetea hakutenda kosa hilo.

Hata hivyo alikiri kuwepo tafrani iliyosababishwa na marehemu aliyekuwa mlevi baada ya kumpiga mtoto wake wa kiume kwa jiwe.

Jaji alisema ni kweli mshitakiwa alitakiwa kulinda familia yake, lakini hakutakiwa kutumia nguvu kubwa aliyoitumia na ushahidi uko wazi kuwa kiini cha ugomvi sio mshitakiwa bali marehemu aliyempiga mtoto wa mshitakiwa.

Kutokana na ukweli huo,  alimtia hatiani kwa kosa la kuua pasipo kukusudia na kumhukumu kifungo cha miaka 10 jela.

Related Posts