Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa fedha za miamala, Edgar Edson Mwakabela maarufu kama Sativa, ametoa notisi ya siku 90 ya kuwashtaki Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, akidai kulipwa fidia ya Sh5 bilioni kwa maumivu ya mwili, utesaji na udhalilishaji aliofanyiwa.
Notisi hiyo ambayo Mwananchi imeiona imetolewa na Sativa kupitia kwa mawakili wake Tito Magoti na Jebra Kambole chini ya kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Mashtaka dhidi ya Serikali, Sura ya 5 ya 2019.
Mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wametoa tahadhari kwamba, iwapo fidia hiyo haitalipwa ndani ya siku 90, wataanzisha kesi ya madai.
“Pia tutawasilisha malalamiko kwenye vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu, ili kuhakikisha haki ya mteja wetu inapatikana,” imeeleza notisi hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alipotafutwa kwa simu jana Jumamosi Septemba 21, 2024, amesema suala hilo linapaswa kujibiwa na Wakili Mkuu wa Serikali.
Mwananchi lilimtafuta Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi, naye alijibu: “Sina taarifa waulize wenyewe mawakili.”
Juhudi za kuwapata IGP, Camillius Wambura na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Ally Gugu hazikufanikiwa baada ya namba zao kutopatikana kila walipopigiwa.
Hata hivyo, notisi hiyo inaonyesha imesainiwa kupokelewa katika ofisi za IGP, pia imepokelewa kwa mhuri katika ofisi ya AG Dodoma na kupokelewa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mhuri zote Septemba 19, 2024.
Sativa alitekwa na watu wasiojulikana Juni 23, 2024 akiwa Kimara, jijini Dar es Salaam na kupatikana Juni 27, 2024 katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi mkoani Katavi akiwa na majeraha.
Baada ya hapo alichukuliwa hadi Dar es Salaam na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan.
Katika maelezo yake, Sativa amedai alipochukuliwa na watu hao alipelekwa kituo cha Polisi Oysterbay, madai ambayo polisi wamesema wanayachunguza.
Awali, Juni 27, 2024 Kamanda wa Polisi mkoani Katavi, Kaster Ngonyani alisema wanafanya uchunguzi wa kuokotwa kwa Sativa.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema taarifa ya uchunguzi ilishatolewa.
“Polisi ni taasisi na jambo lile kama alivyosema kamanda wa Katavi na alisema vizuri tu na ninaamini uchunguzi kupitia yeye unafanyika,” alisema.
Katika notisi ambayo Mwananchi imeiona, mawakili Jebra Kambole na Tito Magoti wamedai mteja wao amefanyiwa ukiukwaji mkubwa wa haki zake.
Wamedai alipata maumivu ya mwili, mateso na kudhalilishwa ambako alikumbana nako akiwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi linalofanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
“Tumeelekezwa na mteja wetu kuwajulisha taarifa ya kisheria ya siku 90 kama inavyohitajika chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mashtaka dhidi ya Serikali ya mwaka 2019,” amesema.
Wamedai Juni 23, 2024, mteja wao alipokuwa akiendelea na shughuli zake halali, alikamatwa ghafla, kushambuliwa na kutekwa na watu wanne waliokuwa wamevaa mavazi ya kiraia huko Kimara, Wilaya ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam.
“Baada ya kutekwa, mteja wetu alilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Noah. Aliwekewa pingu, kufungwa macho na kusafirishwa hadi Kituo cha Polisi Oysterbay, ambapo alifungwa kwenye gogo ndani ya eneo maarufu kama “garage” au chumba cha mateso,” wamedai.
Wamedai Sativa alipokuwa Oysterbay, hakuambiwa haki zake wala kosa aliloshukiwa kufanya, na hivyo kumfanya kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.
“Mteja wetu alitambua wazi mazingira ya Kituo cha Polisi cha Oysterbay alipofunguliwa macho, na alithibitisha kuwa eneo alilokuwa limefungwa kwenye gogo lilikuwa ndani ya kituo hicho cha polisi,” imedai notisi hiyo.
Wamedai mteja wao alikosa huduma muhimu za kibinadamu, akalazimika kujisaidia mwenyewe, hali iliyosababisha mateso makubwa ya kimwili na kiakili.
Notisi hiyo imedai kuwa asubuhi ya Juni 24, Sativa alifunguliwa pingu na kuhamishiwa eneo lisilojulikana.
“Hatimaye alipelekwa Arusha na kufungwa kwenye kituo cha polisi kwa siku kadhaa, huku akiendelea kuteswa na kuhojiwa.
“Juni 25 alipelekwa kwenye msitu ulio mbali na Arusha na kupigwa kwa kutumia mapanga, fimbo na magogo kwa zaidi ya saa tano.
“Alihojiwa kwa nguvu juu ya madai ya kushiriki katika kususia kwa wafanyabiashara wa Kariakoo na kuhusika kwake na wanasiasa wa upinzani,” imedai notisi hiyo.
Imeendelea kudai kuwa, baada ya mateso hayo, alipelekwa Sumbawanga, eneo la Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ambapo alipigwa risasi shavuni karibu na uso wake upande wa kulia.
“Alitelekezwa kwenye mto unaojulikana kuwa na wanyama hatari, lakini baadaye aliokolewa na wapita njia.”
“Kwa msingi wa ukweli huo, tunadai fidia ya Sh5 bilioni kwa majeraha ya mwili, mateso ya kiakili, gharama za matibabu na hasara za kiuchumi,”imeeleza sehemu ya notisi hiyo.