Simba, Dodoma Jiji kupigwa Jamhuri

HATIMAYE Uwanja wa Jamhuri, Dodoma umerejeshwa katika orodha ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/2025, baada ya kufanyiwa maboresho katika maeneo ambayo yalisababisha upoteze sifa zilizoainishwa kwenye kanuni na sheria za mpira wa miguu.

Tamko hilo la Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ambalo lilitolewa jana, Jumapili limeifanya Dodoma Jiji kuwa na uhueni ya kuendelea kucheza michezo yake ya kimshindano ikiwa nyumbani.

Na kwa mujibu wa ratiba Jumapili ijayo, Septemba 29, Dodoma Jiji wataikaribisha Simba kwenye hekaheka za ligi Kuu Bara.

Taarifa ya kufunguliwa kwa uwanja huo, imeeleza; “Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa maboresho ni pamoja na eneo la kuchezea (pitch), mabenchi ya ufundi na uzio unaotenganisha mashabiki na eneo la kuchezea.

“Kwa taarifa hii na kwa mujibu wa Kanuni ya 9:8 ya Ligi Kuu kuhusu Uwanja, Bodi inautaarifu umma kuwa michezo ya nyumbani ya klabu ya Dodoma Jiji iliyopangwa kuchezwa baada ya Septemba 28, 2024

itafanyika katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma kama. ilivyoainishwa kwenye ratiba mama ya Ligi Kuu.”

Kwa upande wa meneja wa Uwanja huo, Anthony Nyembera alisema; “Tumejitahidi kufanya kila ambacho kilikuwa kikihitajika ili uwanja wetu kukidhi vigezo husika, tuna mikakati mbalimbali ambayo tunaamini itatusaidia uwanja kuendelea kuwa katika hali nzuri.”

Awali uwanja huo uilifungiwa na Bodi ya Ligi na kuilazimisha Dodoma Jiji kuhamia kwa muda kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati, Manyara.

Related Posts