SHIRIKA la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan (MAFF) na sekta binafsi chini ya makampuni makubwa ya Japan yanayojishughulisha na kahawa ya UCC Holdings na Marubeni; zilizindua utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya sekta binafsi na wakulima wadogo wa zao la kahawa ambapo, Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya kwanza na ya mfano katika utekelezaji wa Mpango huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo. Amelitaja kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo, linatumika kibiashara kwa kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 34 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan. Takwimu hizo zinaiweka Japan kuwa mnunuzi mkubwa na namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.
Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Mitsuo Takahashi, Naibu Waziri wa Kilimo, Misitu na Uvuvi wa Japan, anayehusika na Masuala ya Bunge la Japan, katika hotuba yake alieleza kuwa Japan na Tanzania ni washirika wakubwa wa maendeleo hususan, katika sekta ya kilimo. Alibainisha kuwa Japan inaitambua Tanzania kwa uzalishaji wa kahawa yenye ubora ambayo, imejizolea umaarufu na kuwa miongoni mwa kahawa tatu bora nchini humo. Kwa umuhimu huo, alieleza kuwa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na sekta binfasi kupitia makampuni ya Marubeni na UCC Hodlings imedhamiria kutekeleza Mpango wa ELSP unaoratibiwa na Shirika la IFAD kuliongezea thamani na uzalishaji zao hilo kwa kuboresha mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo wa kahawa kusini mwa Tanzania, katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma.
Aidha, Waziri Takahashi, alielezea chimbuko la Mradi huo kuwa mnamo mwezi Aprili 2023, Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi (MAFF) ya Japan ilitangaza kuanza utekelezaji wa ‘Mapango wa Ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Wazalishaji Wadogo (ELPS)” ukiwa ni moja ya maazimio yaliyopitishwa na Marais wa Nchi zenye Nguvu Kiuchumi Duniani wa Kundi la G7 kwenye Mkutano wao uliofanyika jijini Hiroshima, Japan.
Vilevile, kwa upande wake Bi. Gerardine Mukeshimana, Makamu wa Rais wa IFAD, aliuelezea Mpango wa ELPS unaotekelezwa na Shirika hilo, kuwa unalenga kubadilisha kilimo cha wazalishaji wadogo kwa njia endelevu kwa kuboresha uzalishaji wao na upatikanaji wa soko kwa kuchochea ushiriki wa sekta binafsi na uwekezaji katika kilimo na mifumo ya chakula. Alieleza kuwa Mpango huo una lengo mahsusi katika kuunganisha wazalishaji wadogo na makampuni ya sekta binafsi, kutumia mitandao ambayo IFAD imeianzisha katika maeneo ya vijijini kwa nchi zinazoendelea. Hivyo kufuatia lengo hilo, alifafanua kuwa IFAD, kwa ushirikiano wa karibu na MAFF na kampuni za UCC na Marubeni, imeanzisha Mradi wa Kwanza wa Majaribio wa Mpango huo na kuwa nchi iliyochaguliwa ni Tanzania kupitia zao la kahawa; Mradi huo utasaidia vyama tisa vya ushirika vya wakulima Tanzania (AMCOS) katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma, utakaogharimu takriban Dola za Marekani 460,000.
Mwishoni mwa mwezi Juni hadi mapema Julai 2024, IFAD pamoja na UCC na Marubeni, zilifanya ziara nchini Tanzania ili kutekeleza Mpango wa ELPS kwa uwekezaji wa pamoja. Tukio la Uzinduzi wa Mpango huo lililofanyika Tokyo, Japan, tarehe 20 Septemba 2024, limelenga kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya wadau hao wakubwa ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa. Pia, kwa upande wa Japan, uzinduzi huo umelenga kuweka Mpango wa ELPS kuwa ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi; na kwa upande wa IFAD, uzinduzi huo umelenga kukuza maslahi na mahitaji miongoni mwa washirika watarajiwa wa sekta binafsi pamoja na Serikali za Kundi la G7 hususan, katika kuujengea uwezo Mpango wa ELPS.