NA EMMANUEL MBATILO, LINDI
UJENZI wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Ndaki ya Kilimo Kampasi ya Lindi unaoendelea kujengwa Ngongo Manispaa ya Lindi kupitia mradi wa HEET umefikia asilimia 23 ikiwa ni miezi mitatu tangu kuanza kwa ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni katika mradi huo, Naibu Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) Dkt. Liberato Haule amesema ujenzi huo utakapokamilika kampasi hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua Jumla ya wanachuo 800 kwa wakati mmoja.
Amesema Mradi huo unalenga kuleta mageuzi katika elimu ya juu ili kuongeza mchango kwenye uchumi wa Nchi kwa kuboresha mazingira ya kujisomea , kufanya maboresho ya mitaala ya vyuo vikuu na kuongeza wahitimu wanaoendana na soko la ajira .
Kwa upande wake Mhandisi Mkuu wa Mradi huo Bahati Thomas amesema licha ya mradi huo kwenda kwa kasi ila kuna changamoto ya ucheleweshaji wa material kama mchanga,kokoto na saruji hali inayopelekea kuchelewa kwa baadhi ya hatua.
Nae Mtendaji wa mtaa wa Kiduni ambapo mradi unaendelea, Rajabu Mpili ameipongeza serikali kwa kuwapelekea chuo hicho ambacho ni cha kwanza kwa ukubwa mkoani Lindi.
Amesema hadi sasa kuna zaidi wa wananchi 200 ambao wamenufaika kwa kupata kazi na hali iliyopelekea kuinuka kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja.