Ikiwa unamiliki gari kwa muda mrefu siku likipata hitilafu ukalazimika kuliacha na kutumia usafiri wa umma, bila shaka utapata usumbufu na karaha.
Hilo litakufanya ulitengeneze gari haraka ili uendelee na maisha ya kutosukumana na watu kwenye usafiri wa umma, kuwahi kazini na pengine kumaliza mizunguko yako ya kutafuta maisha kwa wakati.
Ila leo ni siku ya kimataifa ya kutembea bila gari (binafsi), kwa kimombo inaitwa ‘Car Free Day.’
Kila ifikapo Septemba 22, dunia huadhimisha siku ya kutembea bila gari kuwahimiza madereva duniani kote kuachana na magari yao kwa siku moja. Lengo la siku hii ni kutathimini maisha bila magari barabarani.
Watu wengi duniani wanachukulia magari ni muhimu sana. Pasipo gari, wangeweza vipi kufika mahali mahususi kwa urahisi? Kwa sasa, takriban magari bilioni 1.4 yanatumika katika barabara mbalimbali duniani. Wakati fulani, Marekani ilikuwa na waendeshaji wengi wa magari lakini sasa China inachukua sifa hiyo. Kampuni kama Volkswagen na Toyota zinatengeneza magari zaidi kuliko nyingine.
Ingawa magari yanatoa njia rahisi ya kusafiri, yana madhara kwa mazingira. Mbali na kuchafua hewa, wataalamu wanabainisha kuwa yanachangia katika ongezeko la joto duniani.
Siku hii inawahamasisha madereva kutembea kwa miguu au kuendesha baiskeli.
Inakuza matumizi ya usafiri wa umma kwa wale wanaohitaji kusafiri umbali mrefu. Pia ni siku ambapo miji inaweza kutumia barabara zake kwa njia tofauti.
Jinsi ya kusherehekea siku ya kutembea bila gari, Kwa mfano, katika Sao Paulo, Brazil, siku ambayo wengi hutumia farasi kwa usafiri.
Pia mnaweza kuandaa sherehe za kula chakula barabarani na matukio mbalimbali ya kujifurahisha.
Pia hakikisha unaungana na wengi kutotembea kabisa na gari lako. Ikiwa unahitaji kwenda mahali fulani, tembea au panda baiskeli.
Hii pia ni siku salama zaidi kwa wanaotumia skateboard au scooter ya umeme, kwa kuwa barabara hazitakuwa na magari mengi ni nafasi pia kwa baadhi ya maeneo hasa yanayomilikiwa na majiji kufanya matangazo ya bidhaa kwenye maeneo ya barabara.
Pia inaweza kutumika kama fursa ya kutoa elimu kuhusu uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya magari.
Faida ya hii siku ni kufanya mazoezi ya mwili kwa kutembea, kupunguza gharama, kujifunza kupata uzoefu wa wanaotumia usafiri wa umma,
Unaweza kutueleza ulichojifunza ulipotumia usafiri wa umma.
Historia ya Siku ya Kutembea Bila Gari Duniani
Tangu miaka ya 1950, kuna vikundi mbalimbali vilivyoandamana dhidi ya matumizi ya magari. Wakati huo, waliona magari kama uvamizi katika miji na maeneo yao. Kuanzia mwaka 1956 hadi 1957, Uholanzi na Ubelgiji zilifanya siku za Jumapili ni a kutembea bila magari.
Katika miaka hiyo, tafiti zilianza kuonyesha athari hasi za magari kwa mazingira. Katika mkutano wa kimataifa mwaka 1994, karatasi iliyoelezea mkakati wa kupunguza utegemezi wa magari iligawanywa.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, miradi ya kutembea bila magari ilipangwa na kutekelezwa katika miji mbalimbali ya Ulaya. Mwaka 1997, Chama cha Usafiri wa Mazingira cha Uingereza kiliratibu siku tatu za kila mwaka za kutembea bila gari. Hispania, Italia, na Ufaransa zilitilia maanani miradi kama hiyo.
Tangu wakati huo, imekuwa tukio la kila mwaka kwa nchi 46 na miji 2,000 kote duniani.