Wawili wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kuwaua watalaka wao

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Kanda ya Kigoma, imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa wanaume wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya mauaji ya waliokuwa wake zao.

Hukumu hizo zimetolewa Septemba 19 na 20, 2024 na Jaji John Nkwabi, aliyesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha makosa pasipo kuacha shaka.

Edward Basesegwa, alihukumiwa kwa kosa la kumuua aliyekuwa mke wake, Helena Nzeluke.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, watoto wa marehemu walimkuta mama yao akiwa amelala kwenye dimbi la damu iliyokuwa ikitoka kichwani akiwa na majeraha matatu.

Katika utetezi, Edward alikana kugombana na Helena akidai mtoto wa marehemu ndiye aliyemshawishi mama yake kumuacha.

Aliieleza Mahakama asingeweza kumuua Helena kwa sababu amewahi kuachana na wanawake wengi warembo.

Edward alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba, mshtakiwa akiwa na mashahidi wanne.

Ilidaiwa Edward na Helena waliachana na usiku wa siku ya tukio Oktoba 16, 2022, watoto wa kiume walikutana na Edward njiani akitoka nyumba aliyokuwa akiishi mama yao ila hawakuzungumza naye, kwa sababu hakuwa akiishi na mama yao na walidai walimtambua kwa sababu kulikuwa na mbalamwezi.

Inadaiwa mshtakiwa alirusha kitu cha kudhuru kinachojulikana kwa jina la  ‘moko’ hivyo walikimbia.

Walidai walipofika ndani walimkuta mama yao amelala kwenye dimbwi la damu iliyokuwa ikimtoka kichwani akiwa na majeraha matatu na kupoteza fahamu.

Mtoto mkubwa wa marehemu, Paschal alikimbia kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na kumtaja Edward kuwa ndiye mtuhumiwa akapewa fomu ya polisi namba tatu (PF3) kwa ajili ya matibabu ya mama yake.

Ushahidi unaeleza mama yake alipelekwa kituo cha afya alikopewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na Oktoba 17, 2022 alifariki dunia.

Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alibaini chanzo cha kifo kilikuwa ni kupoteza damu nyingi.

Edward katika utetezi alidai alikuwa akiishi peke yake na Helena alikuwa akiishi karibu na Kituo cha Polisi Gwanumpu.

Alidai shahidi wa pili (mtoto wao wa kiume) ndiye alimshawishi mama yake aachane naye.

Edward alidai asingeweza kumuua Helena kwa sababu amewahi kuachana na wanawake wengi warembo, huku akikana kukamatwa chini ya mti wa parachichi.

Alidai askari polisi wakiwa na mgambo walienda nyumbani kwake ambako alieleza walimpiga kichwani akakimbia ili kwenda hospitali kupata matibabu, lakini alianguka akakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi na baadaye hospitali kwa matibabu.

Jaji Nkwabi amesema amezingatia ushahidi wa pande zote mbili na kujiridhisha kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha pasipo shaka kuwa mshitakiwa ndiye aliyempiga Helena na kusababisha kifo chake.

Amesema ushahidi wa shahidi wa pili Edward, unaonyesha mshtakiwa alikuwa akimpiga Helena walipokuwa wakiishi pamoja kama mke na mume. Pia kulikuwa na ugomvi kati ya mshitakiwa na Helena aliyemtishia kuwa siku moja atamuua.

Jaji amesema licha ya Edward kudai ni mtu mwenye tabia njema, inatisha kwa nini alijigamba kuwa ameachana na wanawake wengi.

Amesema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Septemba 20, 2024 Jaji Nkwabi alimhukumu Miburo Mussa, adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kumkata kwa panga Nemeimana Jacqueline, aliyekuwa mke wake.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Agosti 17, 2020 Jacqueline alifariki dunia baada ya kupata majeraha ya kukatwa kichwani, bega la kulia na kiganja huku vidole viwili vikikatwa.

Daktari aliyechunguza mwili wa marehemu alisema majeraha yaliyotokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali, yalisababisha kuvuja damu nyingi.

Mashahidi wa upande wa mashtaka akiwemo mwanamume aliyemuoa Jacqueline baada ya kuachana na Miburo, walidai kushuhudia mshtakiwa akimjeruhi kwa kutumia panga.

Katika utetezi, Miburo alidai kushangazwa na shtaka hilo, akieleza siku ya tukio hakufika eneo hilo na alitumia siku nzima kujenga nyumba ya mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na baadaye alielekea msikitini kuswali jioni.

Alidai mume wa Jacqueline alikuwa na chuki naye kwa sababu ya mgogoro wa mpaka wa shamba, akieleza alitozwa faini ya Faranga ya Burundi 50,000. Alidai hakuwahi kumuoa wala kumuua Jacqueline.

Jaji Nkwabi amesema ameridhika kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka umejibu kwa uwazi swali la msingi kama mshtakiwa ndiye aliyempiga marehemu.

Amesema baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka walidai kumuona mshtakiwa akimjeruhi marehemu kwa panga akiwa amevaa kanzu nyeupe.

Ilidaiwa mshtakiwa aliwahi kumtishia Jacqueline kuwa atamkatakata vipande.

Mashahidi kadhaa wakiwamo mgambo katika kambi ya wakimbizi walitoa ushahidi huo.

Jaji amesema utetezi wa mshtakiwa kuwa hakukamatwa akiwa na panga, kipande hicho hakikubaliki kwani alikamatwa mchana na miongoni mwa waliomkamata walikuwa viongozi wa eneo hilo ambao ni huru zaidi kuliko mume wa marehemu.

Jaji Nkwabi amesema hoja ya mshtakiwa kwenda kusali asubuhi na jioni, na kwamba hakukutana na mtu yeyote ambaye angemwita kutoa ushahidi kuunga mkono utetezi wake, ni uongo unaothibitisha kesi ya upande wa mashtaka.

Amesema ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka na unaungwa mkono ya ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu.

“Kuhusu nia mbaya ya mshtakiwa, katika kesi hii mshtakiwa alimpiga marehemu mara tatu kichwani kwa kutumia panga, hiyo inatosha kumaanisha kwamba alikuwa na nia mbaya ya kumuua.

“Sihitaji kuzingatia mambo mengine,  kwa sababu hiyo pekee kuhusu mtuhumiwa kutumia kitu chenye ncha kali kumkata marehemu mara tatu kichwani,  kunathibitisha kuwa mtuhumiwa alikuwa na nia ya kumuua,” amesema.

Jaji amesema baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa mauaji,  inamhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Related Posts