WINGA wa Sisli Yeditepe inayoshiriki Soka la watu wenye Ulemavu Uturuki, Mtanzania Shedrack Hebron amesema wanapokutana wabongo wawili kuna bato sio la kawaida.
Hebron anacheza ligi moja na Mtanzania mwenzake, Ramadhan Chomelo anayeichezea Konya na wakikutana wakiwa na timu zao inakuwa na bato la kipekee.
Nyota huyo wa timu ya Taifa ya Walemavu ‘Tembo Warriors’ aliliambia Mwanaspoti wanapokutana uwanjani kila mmoja anapambana kuhakikisha timu yake inapata ushindi na hata mmojawapo asipomfunga basi lazima atatoa asisti ya bao.
“Unajua mkikutana wote Watanzania na mnajuana udhaifu na ubora wa kila mmoja, hivyo lazima kuwe na bato. Mimi nimeifunga timu ya Chomelo mara tatu na assist nne,” alisema na kuongeza.
“Kwa upande wangu napenda sana kutoa asisti kuliko kufunga lakini ikitokea nimeweka mpira nyavuni inakuwa nzuri pia.”
Hebron alijiunga na timu hiyo msimu wa 2022/23 na msimu huo aliifungia klabu yake mabao 10 na asisti 12 huku msimu uliopita akifunga mabao manane na asisti 10.
Kuhusu maandalizi ya msimu mpya, Hebron alisema “Ligi inaanza mwezi ujao na sasa niko mapumziko Dar na natarajia kusafiri mwanzoni mwa mwezi wa 10.”