Beki wa Al Ahly Tripoli ya Libya, Thienry Manzi amemuomba radhi kiungo wa Simba, Deborah Fernandez, baada ya kumuumiza kwenye mchezo wa jana wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya mtoano.
Tukio hilo lilitokea kipindi cha pili ambapo Manzi alionekana kumkanyaga Deborah baada ya wawili hao kuangushana wakati wanawania mpira.
Kwenye tukio hilo licha ya kuonekana na hatari mwamuzi Abdoulaye Manet kutoka Guinea  alimuonyesha kadi ya njano Manzi ingawa wengi waliona alihitaji kupewa kadi nyekundu.
Hata hivyo Manzi ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, akimuomba radhi Deborah kwa tukio hilo.
Manzi ambaye ni raia wa Rwanda ameandika kuwa hakukusudia kumuumiza Deborah na kwamba anashukuru hakupata madhara makubwa.
“Kaka Fernandez (Deborah) imani yangu unaendelea vizuri na samahani kwa tukio lililotokea jana kwenye mechi, sikumaanisha kutaka kukuumiza na wala sikukusudia,” ameandika Manzi huku akiongeza:
“Namshukuru Mungu hukuumia sana. Nakutakia kila la heri kwenye kipaji chako na Mungu akubariki, nawatakia kila la heri na  Wanasimba.”
Mchezo huo ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, ikifanikiwa kutinga hatua ya makundi huku Ahly ikitupwa nje.