Beki Simba haonekani kambini | Mwanaspoti

WAKATI sakata la mshambuliaji wa Simba Queens, Aisha Mnunka likiwa bado halijaisha, limejibuka jipya kuhusu beki wa timu hiyo Mkongomani Daniella Ngoyi ambaye naye haonekani klabuni na hajatoa taarifa.

Daniella anakuwa mchezaji wa pili kuondoka kambini bila taarifa baada ya awali Aisha ambaye tangu Simba Queens itangaze hawamuoni, bado hajatokea kikosini hapo.

Simba Queens ipo Bunju jijini Dar es Salaam ikijifua kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL)inayotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Kabla ya kuingia kambini wiki iliyopita, Simba Queens ilitoa mapumziko ya wiki moja kwa wachezaji baada ya kutoka kwenye michuano ya Cecafa, huku beki huyo ikidaiwa hajajiunga na wenzake.

Taarifa za ndani ya Simba zinaeleza nahodha huyo wa timu ya taifa ya wanawake ya DR Congo, amebeba kila kitu chake kilikuwepo kambini na viongozi hawana taarifa yoyote juu ya kuondoka kwake.

“Viongozi wamewasiliana naye karibu wiki sasa lakini simu haipatikani na hata watu wake wa karibu hawajui alipo,” ilisema taarifa hiyo

Mtu wa karibu na nyota huyo, ameliambia Mwanaspoti kwamba: “Aliniaga anakwenda Congo akiahidi atarudi, sasa sijajua hayo mengine licha ya kwamba muda mrefu umepita.”

Alipotafutwa Meneja wa Simba Queens, Seleman Makanya ili kuzungumzia sakata hilo, simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa. Hii sio mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kutoonekana kambini kwani iliwahi kutokea mwaka 2022 akiwa na Yanga Princess kabla ya kuibukia Simba Queens msimu wa 2022-2023.

Related Posts