Dar es Salaam. Eneo la kuzunguka Soko la Kimataifa la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, shughuli mbalimbali za kiuchumi zinaendelea, huku kukiwa na idadi ndogo ya wateja.
Mpaka kufikia mchana wa saa 7:30 leo Jumatatu Septemba 23, 2024 maduka mengi kuzunguka eneo hili yalikuwa yamefunguliwa na biashara kuendelea kama kawaida. Badhi ya maduka bado hayajafunguliwa.
Mmoja wa wafanyabiashara amelalamikia biashara kudorora kwa siku ya leo, akisema maduka ya bidhaa za jumla ndio chanzo cha biashara nyingi kusimama, licha ya wateja pia kupungua.
Mfanyabiashara huyo, Juma Othman amesema tishio la uwepo wa maandamano ya Chadema ndiyo chanzo cha soko hilo kutokuwa na wateja wengi siku ya leo.
“Jumatatu ni siku iliyochangamka hapa Kariakoo, kwa kuwa maduka ya jumla huuza kwa wingi bidhaa na wateja wa jumla huwa wengi, leo wamepungua sana. Mzunguko wa watu umekuwa mdogo na hata mzunguko wa kifedha umepungua,” amesema Juma.
Baadhi ya wachuuzi wa bidhaa ndogondogo wamesema idadi ya wateja imepungua.
“Kwa leo biashara imedorora, ijapokuwa tunauza lakini nahisi wateja wameogopa kuja kuhofia maandamano, awali polisi walikuwa wakizunguka Kariakoo, lakini kwa sasa wameondoka, ni wachache tunawaona,” amesema mchuuzi huyo wa vijora, Amina Hassan.
Aidha, polisi wanaofanya doria eneo la Kariakoo wamepungua mpaka kufikia saa 7:40 mchana ikilinganishwa na idadi kubwa iliyokuwepo asubuhi.
Ulinzi huo ulitokana na uwepo wa taarifa ya Chadema kufanya maandamano ya maombolezo na amani, jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Polisi imeyadhibiti maandamano hayo na baadhi ya wanachama pamoja na viongozi wamekamatwa.
Miongoni mwa waliokamatwa ni mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Makamu wake-Bara, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
Eneo la kuzunguka Fire, pia shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida, huku kukiwa na idadi ndogo ya watu.