Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la dhamana ya Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai kutokana na kutokuwepo mahakamani.
Jacob, mkazi wa Msakuzi, mfanyabiashara na mwanasiasa anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Alhamisi, Septemba 19, 2024, na upande wa mashtaka pamoja na mambo mengine, uliiomba Mahakama izuie dhamana yake kwa madai ya usalama wake mshtakiwa, hoja zilizopingwa na jopo la mawakili wake likiongozwa na Peter Kibatala.
Baada ya mvutano wa hoja za mawakili, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga aliahirisha mpaka leo Jumatatu, Septemba 23, 2023 saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya dhamana lakini Boni Yai hakufikishwa mahakamani.
Hivyo Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo mpaka Alhamisi, Septemba 26, 2024.