UKIMGUSA shabiki wa Yanga atakukera na maneno yao ya tambo juu ya kutinga makundi kibabe tena mara ya pili mfululizo, ikiwang’oa CBE ya Ethiopia kwa mabao 7-0 na sasa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ametamka anataka timu yake iwe hivyo.
Kocha Gamondi ameliambia Mwanaspoti, kikosi chake kimecheza kwa kiwango bora na kwamba namna hiyo ndivyo anatamani timu yake icheze kwa ubora huo.
Gamondi amesema wachezaji walionyesha kuwa na njaa kubwa ya ushindi huku pia wakicheza kwa nidhamu kubwa ya mchezo kuhakikisha wapinzani wao hawaleti madhara kwenye lango lao.
“Hii timu (CBE) ilikuja na mabadiliko makubwa tofauti na tulivyokutana kwenye mchezo wa kwanza, lakini tuliwaweka kwenye wakati mgumu hasa kipindi cha pili, tulijua watatupa nafasi ya kufanya mashambulizi makali,” amesema Gamondi.
“Kitu kikubwa ambacho kimenifurahisha kwenye mechi ya leo (jana usiku) ni namna wachezaji wangu walivyoonyesha kuwa na njaa ya ushindi mkubwa nadhani ilichangiwa na matokeo yetu yaliyopita.
“Ukiacha kutengeneza ushindi huo pia tulikuwa vizuri kwenye ulinzi, unajua wapinzani wetu hawakupata nafasi ya kupiga shuti lolote lililolenga lango kwetu, natamani wakati wote tuwe tunacheza kwenye ubora kama huu.”
Kocha wa CBE Sisay Kumbe, amekubali mziki wa Yanga akisema timu yake ilikutana na timu ambayo sio levo zao.
Kumbe amesema Yanga baada ya kuwang’oa CBE, ina nafasi ya kwenda kufanya makubwa katika hatua inayoendelea kwa kuwa kikosi chao kina wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
“Ilikuwa mechi ngumu kwetu, tulikutana na timu ambayo haikuwa kwenye uwiano sawa kwetu kwa uzoefu na hata ubora, walistahili kufuzu nawatakia kila la kheri,” amesema Kumbe.
“Timu yangu haina uzoefu mkubwa na mechi kubwa kama hizi, tumejifunza, Yanga nadhani wanakwenda kufanya vizuri zaidi huko mbele kwa uzoefu ambao wachezaji wao wameonyesha na ubora wao watafika mbali.”
Yanga imefuzu makundi ikiungana na vigogo, Al Ahly na Pyramids za Misri, CR Belouizdad na MC Alger za Algeria, TP Mazembe na AS Maniema za DR Congo, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Esperance ya Tunisia na Raja Casablanca ya Morocco.