Dar es Salaam. Kawaida jiji la Dar es Salaam watu huanza pilikapilika kuanzia saa nane hadi saa tisa usiku.
“Wanaokwenda shule na kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi kule Feri, Kariakoo na meeneo mengine wameshaenda na hali ni shwari.
“Wanaokwenda hospitali nao wanaendelea na zile safari zao. Kwa ujumla, shughuli mbalimbali zinaendelea vizuri kama kawaida. Mpaka muda huu, hali ni shwari kabisa.”
Hiyo ni kauli ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliyoitoa leo Jumatatu Septemba 23, 2024 alipozungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika leo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mulilo amesema; “Kwanza sidhani kama hawajalielewa vizuri lile katazo ambalo limefanywa na Jeshi la Polisi.
“Kama watakuwa wanafanya kutoelewa, wataeleweshwa kwa vitendo, kuwa hili katazo limeshatolewa na mnachokifanya ni kinyume na sheria.”
Ameongeza kuwa; “Kutokana na matamshi ya baadhi ya viongozi ambayo yametolewa mara kadhaa, ambayo kimsingi yalikuwa yanaashiria kupelekea kuwa na maandamano ambayo sio ya amani. Kwa sababu sisi kazi yetu ni kufuatilia na kuchunguza, ndiyo maana maandamano yale yalipigwa marufuku. Tunaendelea kuamini hakuna atakayejitokeza.”
Amesema ikitokea mtu akajitokeza kwa nia ya kufanya maandamano ambayo wameyaona yana nia ya uvunjifu wa amani, watamshughulikia kwa hatua kali na za haraka, lakini kwa mujibu wa sheria.
“Ninaona watu mbalimbali wakiwa na shughuli zao, wakiwa katika muelekeo ambao kila mtu anafanya shughuli zake. Kwa hiyo sijakutana na watu ambao walitangaza hicho walichokitangaza kuhusiana na tarehe ya leo ya 23,” amesema Kamanda Muliro.
Amesema Watanzania wenye shughuli mbalimbali wasiwe na hofu. “Wanafunzi waende shule, madaktari waende hospitali, watu wa idara mbalimbali za Serikali na zile ambazo si za serikali waendelee na shughuli zao bila hofu.
“Ulinzi wanaokutana nao ni kwa sababu yao, tumeimarisha ulinzi ili wao wafanye kazi zao na hili ndilo jukumu letu la msingi sisi Jeshi la Polisi.
“Ikitokea wale waliotanganza wakataka kufanya kile walichokitangaza, kwanza sidhani kama watafanya, lakini wakifanya watashughulikiwa vikali na kwa mujibu wa sheria,” amesema Kamanda Muliro.